Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ccm waandamana kumpinga mbunge aliyeitosa Chadema

10742 Pic+ccm TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Kundi la wanachama wa CCM limejitokeza hadharani kupinga aliyekuwa mbunge wa Monduli, Julius Kalanga kurejeshwa kugombea ubunge kupitia chama hicho pasipo kura ya maoni kufanyika.

Julai 31, Kalanga aliyekuwa mbunge kwa tiketi ya Chadema, alitangaza kurejea CCM alikohama mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika.

Kutokana na Kalanga kuhama chama, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), imetangaza uchaguzi mdogo katika jimbo hilo utakaofanyika Septemba 16.

Jana, baadhi ya wanachama wa CCM kutoka kata za Isilalei, Monduli Juu na Sepeko waliandamana hadi ofisi za chama hicho wakimtuhumu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli, Wilson Lengima kwamba kwa kushirikiana na viongozi wengine wa chama, wanapanga njama ili Kalanga apitishwe kuwa mgombea ubunge pasipo kufanyika kura ya maoni.

Hata hivyo, Lengima amekanusha madai hayo akisema CCM ina utaratibu wa kuwapata wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi hivyo kuwataka wana-CCM kuwa watulivu.

Katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni, Dar es Salaam na Siha, Kilimanjaro waliokuwa wabunge (Maulid Mtulia - CUF) na Dk Godwin Mollel - Chadema) waliojiengua na kujiunga na CCM, waliteuliwa pasipo kupitia utaratibu wa kura ya maoni kuwa wagombea.

Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, ilitoa ufafanuzi kuhusu uteuzi wa Mtulia na Dk Mollel kutopitia utaratibu wa kura ya maoni ikisema kanuni za uteuzi wa wagombea wa CCM kuingia katika vyombo vya dola (2010), fungu la tatu, ibara ya 16(2) inasema: “Endapo kwa sababu maalumu, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itaona kuwa hakuna haja ya kuitisha kura za maoni, hususani katika uchaguzi mdogo, itakuwa na uwezo wa kuelekeza kwamba mchakato wa kura za maoni usifanyike.”

Pia, ilifafanua kuwa kanuni hiyo haina mabadiliko na inasomeka vivyo hivyo katika kanuni toleo la 2005 fungu la pili ibara ya 10(2).

Katibu wa uenezi wa CCM Kata ya Sepeko, Nooy Naimisye alisema jana kuwa wanataka kuona demokrasia ikitendeka katika kumchagua mgombea ubunge jimboni Monduli.

“Mwenyekiti atupe ukweli kuhusu madai kwamba yupo upande wa mbunge wa zamani aliyejiuzulu Chadema na kutangaza kujiunga CCM. Tunataka demokrasia, hatuna nia kuona mgombea huyu anagombea tena kwenye chama chetu, hii ni kinyume cha kanuni na utaratibu ndani ya chama,” alisema Naimisye.

Alisema upo utaratibu wa mwanachama kujiunga na CCM na kupewa ridhaa ya kugombea lakini alisisitiza kuwa ndani ya chama hicho kuna utaratibu mzuri wa mtu wa aina hiyo kukaa kwa kipindi fulani kabla ya kuchaguliwa katika nafasi yoyote.

Mwanachama wa CCM kutoka Kata ya Monduli Juu, Daniel Leyani alisema wapewe haki ya kumchagua mgombea wanayemtaka na si kupewa mgombea kwa shinikizo la viongozi.

Mwanachama kutoka Kata ya Esilaley, Sairey Loboye alitaka utaratibu kufuatwa ndani ya CCM akisema mwanachama yeyote mpya akitaka kugombea nafasi za uongozi anatakiwa kuandika barua ya maombi ambayo itajadiliwa na vikao vya chama na kupitishwa au la. Joseph Laizer, mwanachama kutoka Monduli Juu alisema iwapo Kalanga anataka kugombea basi uhuru utolewe kwa wana-CCM wengine kuomba nafasi.

“Hatumpingi Kalanga kwa kuwa tulikuwa naye CCM kabla hajahamia upinzani, aliwahi kuwa mwenyekiti wa UVCCM wa wilaya lakini tunataka utaratibu kufuatwa,” alisema.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare alipotafutwa jana alisema alikuwa kwenye kikao na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally hivyo asingeweza kuzungumzia mgogoro huo.

Viongozi wa mila

Kiongozi wa mila wa Kimasai (Laigwanani) wa kanda ya Manyara, Natuli Letema alisema walimpokea Kalanga na kumpa baraka zao.

“Sisi pia ni wana CCM alikuja Kalanga kwenye kikao chetu, tulikuwa tunajadili migogoro ya ardhi na alitueleza dhamira yake kurudi CCM tukamkubali,” alisema.

Alidai wanaompinga wanatumiwa na mwanasiasa (jina linahifadhiwa kwa kuwa hakupatikana kuzungumzia tuhuma hizo) anayedaiwa aliwakodia magari.

“Monduli ina kata 20 hawa wamekuja kuandamana ni kata tatu watu 40 tunajua wanatumiwa tu,” alisema.

Makada 44 wajitokeza Korogwe

Jimbo la Korogwe Vijijini limeingia katika historia baada ya

makada 44 wa CCM kujitokeza kuwania kupitishwa kugombea ubunge.

Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini, Suraisa Sangusa alisema jana kuwa hatua inayofuata ni kamati ya siasa ya wilaya kuchambua fomu hizo kabla

ya kupeleka majina hayo katika ngazi ya mkoa kwa ajili ya hatua ya

awali ya mchujo.

Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja majina ya waliorejesha fomu na kupokewa

akisema atafanya hivyo kesho.

Jimbo la Korogwe Vijijini limebaki wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake

Stephen Ngonyani (Majimarefu) kufariki dunia mwezi uliopita na Tume ya Taifa

ya Uchaguzi (NEC) imeshalitangaza rasmi kuwa lipo wazi na kuruhusu vyama vya siasa

kuendesha mchakato wa uteuzi wa wagombea.

Chanzo: mwananchi.co.tz