Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF yawadai Maalim Seif, Zitto Sh900 milioni mahakamani

52545 Pic+cuf

Tue, 16 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mpambano wa kisheria baina ya Chama cha Wananchi (CUF) na katibu wake mkuu wa zamani, Maalim Seif Sharif Hamad unazidi kukolea, licha ya kukihama baada ya chama hicho kumfungulia kesi mbili yeye na wenzake, kikiwadai fidia ya jumla ya Sh900 milioni.

Kesi hizo zimefunguliwa na Bodi ya Wadhamini CUF katika Mahakama Kuu Zanzibar na Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya Maalim Seif na wenzake akiwamo Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kikiwadai fidia hiyo kutokana na uharibifu uliofanywa katika ofisi zake.

Katika kesi hizo, chama hicho kinadai kuwa uharibifu huo ulifanywa na mawakala au wawakilishi wa Maalim Seif na wenzake muda mfupi tu baada ya kutangaza kujiunga na ACT-Wazalendo.

Maalim Seif alijiunga ACT-Wazalendo Machi 18 muda mfupi baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu uliomhalalisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF) na siku chache baada ya Baraza Kuu la Uongozi la CUF kutangaza kumvua uanachama yeye na wenzake.

CUF inadai kuwa kufuatia uamuzi huo, Maalim Seif, Zitto na wenzao kwa msaada wa mawakala na au wawakilishi wao, walipaka rangi ya chama cha ACT-Wazalendo katika majengo mbalimbali ya ofisi za CUF, ngazi ya matawi na wilaya Zanzibar na Bara.

Kwa mujibu wa hati za madai, chama hicho kinadai kuwa mawakala na wawakilishi hao wa Maalim Seif na wenzake walifanya uharibifu huo kwa ushauri wa mmoja wa wadaiwa katika kesi hizo, Daimu Halfan, huku wakijua kuwa ni kinyume cha sheria

Uharibifu mwingine unaodaiwa ni kushusha na kuchoma bendera zake na kisha kupandisha za ACT- Wazalendo katika ofisi zake, kuondoa na kuharibu samani na nyaraka za ofisini.

Chama hicho kinapinga madai ya baadhi ya wadaiwa (Mazrui, Faki na Juma) kwamba majengo hayo yalikuwa ni ya watu binafsi waliokuwa wameyatoa kwa chama hicho kumuunga mkono Maalim.

Badala yake, CUF inadai kuwa tangu mwaka 1992, kimekuwa kikimiliki majengo kilipoanzisha ofisi zake katika ngazi za matawi na vijiwe, ambayo kiliyanunua maeneo ya Mabibo na Magomeni Dar es Salaam, Tanga mjini na maeneo mengine Tanzania Bara.

Katika kesi namba 60 iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wadaiwa ni Zitto (mdaiwa wa kwanza), Maalim Seif (mdaiwa wa pili) na wenzao saba.

CUF inadai kuwa uharibifu huo ulifanyika katika ofisi za matawi mbalimbali hususan Mabibo, Magomeni na maeneo mengine Tanzania Bara hivyo kinaomba Mahakama hiyo itamke na kuamuru kuwa matendo na mwenendo wa wadaiwa hao katika ofisi zake ni vya uvamizi na uingiaji wa kijinai.

Pia kinaomba Mahakama iwaamuru na kuwalazimisha wadaiwa, mawakala na au wawakilishi wao kuzirejesha ofisi zao katika hali yake ya awali kama vilivyokuwa na vitu vyote vilivyokuwamo.

Katika mbadala wa maombi hayo, wanaiomba mahakama iwaamuru wadaiwa kulipa Sh200 milioni kama thamani ya samani na nyaraka zilizoharibiwa na fidia ya kupanga rangi ya ACT- Wazalendo katika ofisi zake pamoja na Sh100 milioni kama fidia ya adhabu pamoja na gharama za kesi.

Katika kesi namba 16 ya 2019, iliyofunguliwa Mahakama Kuu Zanzibar Vuga, wadaiwa ni Zitto ambaye ni mdaiwa wa kwanza, Maalim Seif wa pili na wenzao 18.

ambao walikuwa ni viongozi na wanachama wa CUF, waliojiunga ACT- Wazalendo.

Katika kesi hiyo chama hicho kinadai kuwa uharibifu huo ulifanywa katika ofisi zake za matawi na za wilaya katika maeneo mbalimbali kama vile Mtendeni, Vuga, Kilimahewa, Micheweni, Mkoani, Chambani, Nungwi Kaskazini A, Chakechake Pemba na maeneo mengine ya Zanzibar.



Chanzo: mwananchi.co.tz