Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF yatamba kushinda ubunge, madiwani Kigoma mjini

52839 Pic+cuf

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Chama cha Wananchi (CUF) kimeomba wakazi wa Kigoma mjini kuunga mkono harakati zake za kisiasa ili kiibuke na ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Kigoma mjini, Yasin Mambobado, amesema hayo leo Jumatano Aprili 17, 2019 akizungumza na baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji waliokutana na asasi ya Meza ya Duara ya Watanganyika.

Mambobado amesema licha ya mgogoro uliokikumba chama hicho, kimeendelea kuwa imara mkoani Kigoma na kinatarajia kushinda uchaguzi za serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu Mwaka 2020.

"Tumejipanga kushinda wenyeviti wa mitaa wengi mwaka huu na mwaka ujao tushinde madiwani wengi na mbunge hapa Kigoma mjini," amesema Mambobado.

Amesema chama hicho kimekamilika kwa kupata viongozi wa ngazi zote na kilichobakia ni kukijenga ili wananchi waendelee kukiamini na kuchagua wagombea wake.

Naye mwenyekiti wa Meza ya Duara ya Watanganyika, Shukuru Kondo alihoji juu ya wanachama wengi wa CUF kutimkia ACT Wazalendo kama chanzo cha CUF kupoteza matumaini ya watu.

"Nahofia taarifa inayotolewa hapa ni ya uongo kwamba CUF ni imara na itashinda Uchaguzi Wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka ujao, kwani wanachama wanahama sasa huo uimara uko wapi?" amehoji Kondo.

Akijibu swali hilo, Mambobado amewatoa hofu wakazi wa Kigoma mjini kwamba chama chake kipo imara na sasa kimepata viongozi waadilifu wanaokubalika kwa jamii.

"Mkakati wa CUF ilikuwa kujiimarisha kwanza Zanzibar baadaye tuhamie bara lakini baada ya huu mgogoro uliotokea tumeamua kujenga chama bara na visiwani kwa nguvu ileile,  hilo tunalimudu," amesema Mambobado.

Pia, ametumia fursa hiyo kukanusha madai kwamba chama hicho kinatumiwa na Dola kukwamisha harakati za vyama vya upinzani kuing'oa CCM madarakani.



Chanzo: mwananchi.co.tz