Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF yatamba kumng’oa ubunge Zitto Kigoma mjini

52782 Pic+kayanda

Wed, 17 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kigoma. Chama cha Wananchi (CUF) kimeomba wakazi wa Kigoma mjini kuunga mkono harakati za kisiasa za chama hicho ili kiibuke na ushindi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Kigoma mjini, Yasin Mambobado amesema hayo leo Jumatano April 17 wakati akizungumza na baadhi ya wakazi wa manispaa ya Kigoma Ujiji waliokutana katika asasi ya Meza ya Duara ya Watanganyika.

Amesema licha ya mgogoro uliokikumba chama hicho bado kimeendelea kuwa imara mkoani Kigoma na kinatarajia kushinda katika chaguzi za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka ujao 2020 ikiwamo ubunge wa Kigoma Mjini unaoshikiliwa na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

"Tumejipanga kushinda wenyeviti wa mitaa wengi mwaka huu na mwaka ujao (2020) tushinde madiwani wengi na mbunge hapa Kigoma mjini," amesema Mambobado.

Amesema chama hicho kimekamilika kwa kupata viongozi kwenye ngazi zote na kilichobaki sasa ni kujenga chama ili wananchi waendelee kukiamini na kuchagua wagombea kutoka CUF kupitia chaguzi hizo.

"Nitoe wito kwa watu wanaotaka kugombea nafasi za uenyeviti wa mitaa, udiwani na ubunge hapa Kigoma mjini wasisite kufanya hivyo na chama pekee kitakachowafanya kushinda ni CUF," amesema Mambobado.

Mwenyekiti wa Meza ya Duara ya Watanganyika, Shukuru Kondo alihoji juu ya wanachama wengi wa CUF kuhama na kutimkia ACT Wazalendo kama chanzo cha CUF kupoteza matumaini ya watu.

"Nahofia taarifa inayotolewa hapa ni ya uongo kwamba CUF ni imara na itashinda chaguzi za Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka ujao, kwani wanachama wanahama na kuondoka, sasa huo uimara uko wapi?" amehoji Kondo.

Akijibu, Mambobado amewatoa hofu wakazi wa Kigoma mjini akisema chama hicho bado kipo imara na kwa sasa kimepata viongozi waadilifu wanaokubalika mbele ya jamii.

"Mkakati wa CUF ilikuwa kujiimarisha kwanza Zanzibar baadaye tuhamie Bara lakini baada ya kumalizika huu mgogoro uliotokea tumeamua kujenga chama bara na visiwani kwa nguvu ileile na hilo tunalimudu," amesema Mambobado.

Aidha, ametumia fursa hiyo kukanusha madai kwamba chama hicho kinatumiwa na dola kukwamisha harakati za vyama vya upinzani kuing'oa CCM madarakani.

Amesema kila chama kina itikadi, sera na malengo yake, hivyo kusema wanakwamisha upinzani kuingia madarakani ni kukipaka matope CUF.

Mkazi wa Mwanga mjini Kigoma, Hamisi Juma amewataka viongozi wa CUF kufanya kazi ya ziada kukijenga chama hicho ili kikubalike kwa wananchi na hapo kitaweza kutoa ushindani kwa vyama vya ACT- Wazalendo, Chadema na CCM ambavyo vina wafuasi wengi mjini Kigoma.

Chama cha CUF kwa sasa hakina mwenyekiti hata mmoja katika mitaa 68 na hakina diwani katika kata zote 19 zilizopo Kigoma mjini.



Chanzo: mwananchi.co.tz