Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema Jeshi la Polisi kusambaratisha mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho, huku likiwakamata viongozi wake ni ukandamizaji wa demokrasia na haki ya mikusanyiko halali, huku kitaka kiombwe radhi.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Ilala Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi (RPC), Yustino Mgonja hakutaka kuzungumzia tukio hilo kwa undani huku akikiri kuwa taarifa hiyo aliipata tangu asubuhi na anaifuatilia.
“Kamanda wa Kanda Maalumu ataitolea ufafanuzi muda si mrefu, kwa hiyo tusubiri kidogo maelekezo yatatolewa,” amesema ACP Mgonja.
Tukio hilo lilitokea jana Novemba 24,2023 ambapo chama hicho Wilaya ya Ilala kilipanga kufanya mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Buguruni Sheli, baada ya kufuata taratibu zote za kisheria zinazotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuandika barua kwa Mtendaji wa Kata kuomba kuutumia huo uwanja na kuliandikia barua Jeshi la Polisi kulitaarifu wiki nzima kabla ya siku ya tukio.
Akizungumzia tukio hilo, Profesa Lipumba amesema Serikali iliruhusu mkutano huo kufanyika lakini ilipofika saa tisa alasiri, Jeshi la Polisi kutoka Kituo cha Buguruni walivamia na kusambaratisha watu, kukamata viongozi na kuchukua vyombo vya muziki, matangazo pamoja na gari na kuvipeleka kituo cha Polisi.
“CUF, tunalaani kitendo kilichofanywa na Jeshi la Polisi kuvuruga mkutano ulioandaliwa kwa gharama na muda, pia kuwakamata viongozi wetu ambao wamefuata taratibu zote za kuitisha mikutano ya hadhara. Huu ni ukandamizaji wa demokrasia na haki ya mikusanyiko halali,” amesema.
Profesa Lipumba amesema kama kweli Serikali ina dhamira ya dhati katika dhana ya maridhiano basi ni vema ikatambua wanaotegemewa kusimamia utekelezaji wa maridhiano hayo wanaweza kuwa kikwazo kikubwa.
“Unapovunja sheria na kutamba kwamba huogopi mamlaka ni zaidi ya utovu wa nidhamu, hususani maneno hayo yanapotamkwa kwa viongozi wa kisiasa,” amesema.
Pia alitoa wito kwa Serikali kukiomba radhi chama hicho kwa yote yaliyofanywa na jeshi hilo kwa kusababisha hasara ya kuandaa mkutano, kushikilia viongozi na muda waliopoteza kulifuatilia jambo hilo kituoni.