Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF wataka wananchi Ukonga kutochagua mbunge wa majaribio

16052 Cuf+piuc TanzaniaWeb

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimewataka wananchi wa jimbo la Ukonga kutochagua mbunge wa jimbo hilo kwa majaribio.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Septemba 6, 2018 na

mkurugenzi wa mipango na uchaguzi wa chama hicho, Jafar Mneke wakati akimnadi mgombea ubunge wa CUF  jimbo la Ukonga, Salama Masoud  katika mkutano wa kampeni uliofanyika Madafu Ukonga.

Amesema wananchi wa Ukonga mwaka 2015 walifanya majaribio kwa kumchagua mbunge wa Chadema, Mwita Waitara ambaye Julai 2018 alihamia CCM.

“Amewaacha njiani, siasa haijaribiwi kwa sababu ni maisha na ndio inahusika kupanga namna ya kuishi hivyo fanyeni maamuzi sahihi," amesema Mneke.

Amesema CCM imeshindwa kuwakomboa Watanzania na kwamba kwa sasa maisha ya wananchi yapo hatarini, akitolea mfano mambo mbalimbali likiwemo suala la haki za binadamu.

Amesema kwa sasa hakuna mwenye uhakika wa maisha kwa madai kuwa kumekuwa na matukio yanayoharatisha amani.

Kaimu mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Ilala, Hamisi Chambuso amesema wataiandika barua Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuwachunguza wanachama wa vyama vya upinzani wanaohaha kuhamia CCM, wakiwemo wabunge na madiwani.

Amesema licha ya mkurugenzi wa Takukuru kuchaguliwa na Rais, hilo haliwatishi kutaka uchunguzi huo.

"Takukuru walete majibu ya uhakika na wakileta ya kupika wataibua hoja mpya kabisa,” amesema  Chambuso.

Amesema adhabu pekee kwa wananchi wa Ukonga dhidi ya CCM ni kumchagua Salama kuwa mbunge wa Ukonga.

Kwa upande wake  Salama ametaja vipaumbele vyake, ikiwemo afya na kubainisha kuwa vifaa mbalimbali vitatolewa bure, vikiwemo vya kujifungulia.

Amesema kipaumbele kingine ni elimu na kubainisha kuwa atahakikisha hakuna mtoto anakosa masomo kwa kukosa nafasi shuleni.

"Walimu hawana motisha ya kazi  asilimia 70 ya mishahara yao imeshikiliwa na mabenki. Nitahakikisha wanapanda madaraja na kuongezewa mshahara,” amesema.

Mengine aliyoyataja kuwa atayafanyia kazi ni maji, kuboresha miundombinu na huduma kwa wazee.

"Waliofikisha miaka 50 na kuendelea nitawapa bima ya afya bure, haya yote yanawezekana kupitia fedha ya mfuko wa jimbo,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz