Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF wataka tume huru kabla ya Katiba mpya

CUF CUF wataka tume huru kabla ya Katiba mpya

Fri, 6 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Wananchi (CUF) kimesema matamanio yao kwa sasa ni kupatikana kwa tume huru ya uchaguzi kabla ya mwaka 2024 na 2025.

Hayo yameelezwa na Naibu Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Yusuph Mbugiro alipozungumza na waandishi wa habari leo Januari 6 makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini hapa.

Amesema matamanio ya chama hicho ni kuona ikifika mwaka 2024 kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na 2025 kwenye uchaguzi mkuu, tume hiyo ndiyo isimamie na sio Halmashauri.

"Ni rahisi kuunda tume huru ya uchaguzi, kabla ya Katiba mpya tuanze na tume," amesema Mbugiro. Amesema wanaamini kuna uhitaji wa katiba mpya, lakini kabla mchakato wake haujakamilika, ianze kwanza tume huru ya uchaguzi.

"Muundo wake upo kupitia rasimu ya Warioba (Jaji Joseph), CUF tutafanya kazi kuhakikisha inapatikana, tunaomba na wadau wengine watuunge mkono ili lifanikiwe,” amesema.

Hivi karibu Rais Samia Suluhu Hassan alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa Ikulu jijini Dar es Salaam na kuruhusu mikutano ya hadhara, pia aligusia suala la kupatikana kwa katiba mpya na kueleza amedhamiria kuukwamua mchakato.

Mbungiro leo amesema kabla ya katiba mpya, mchakato ambao wanaona utachukua muda mrefu, ipatikane kwanza tume huru ya uchaguzi ambayo CUF wanaihitaji kabla ya chaguzi zijazo.

"Tunamshukuru Rais kuruhusu mikutano ya hadhara, tunatarajia hata hili la tume huru litafanikiwa," amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live