Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF wamuomba Magufuli kuruhusu mikutano ya hadhara

69676 Pic+cuf

Sun, 4 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) nchini Tanzania kimemuomba Rais John Magufuli kutoa tamko la kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumamosi Agosti 3, 2019 na naibu mkurugenzi wa sheria na haki za binadamu wa chama hicho, Salvatory Magafu katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Amesema mikutano ya hadhara ni muhimu kwa ajili ya  viongozi kuzungumza na kusikiliza kero za wananchi, hivyo ni muda muafaka kuruhusu mikutano.

“Tunamuomba Rais John Magufuli atoae tamko la kuruhusu mikutano ya hadhara kwani alipopiga marufuku aliahidi kuruhusu kipindi cha uchaguzi hivyo huu ni muda muafaka,” amesema Magafu.

Katika hatua nyingine mkurugenzi huyo amelitaka jeshi la polisi nchini kuacha kukiuka sheria na lifanye kazi bila ubaguzi wala upendeleo ili kuendelea kulinda amani ya nchi.

Amesema hiyo ni kutokana na baadhi ya wabunge na viongozi wa chama hicho kuzuiwa mara kwa mara kufanya mikutano yao ya ndani pamoja na kuwekwa chini ya ulinzi.

Pia Soma

Chama hicho kimedai kilipanga kufanya mkutano wake Vinguguti lakini umezuiwa.

“Tuliandika barua Julai 29 mwaka huu kuomba kibali cha kufanya mkutano wa hadhara Vingunguti relini tuliandika barua kwa kamanda wa polisi Buguruni kuomba kibali, lakini  jana (Ijumaa Agosti 2) tulipokea barua kutoka ofisi ya mkuu wa polisi Buguruni ya kuzuia mkutano wetu,” ameongeza.

Akizungumza kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Ilala Zuberi Chembela amesema hawakuwakataza kufanya mkutano bali barua haikuandikwa na mhusika.

“Sisi hatuzuii mikutano kufanyika bali tunataka barua ya kuomba kibali itoke kwa mhusika wa eneo ambaye amechaguliwa na wananchi aidha mbunge, diwani au mwenyekiti wa serikali za mitaa,” amesema Chembela.

Naye Mkurugenzi wa mambo ya nje sera na Bunge w chama hicho, Mohammed Ngulangwa amesema lengo la mkutano huo wa hadhara uliopangwa kufanyika leo ilikuwa kukagua uhai wa chama, kuimarisha chama na kufikisha sera ya haki sawa kwa wote.

Chanzo: mwananchi.co.tz