Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF upande wa Maalim Seif walianzisha

45813 Cufpic CUF upande wa Maalim Seif walianzisha

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif  Hamad, wanajipanga kuzuia mkutano mkuu uliopangwa kufanywa na wenzao upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.

Upande huo wa Maalim Seif umesema mkutano huo umepangwa kufanyika kati ya Machi 12 hadi 15, 2019 ambako miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kufanywa ni pamoja na uchaguzi wa viongozi mbalimbali wenye lengo la kumfukuza uanachama Maalim Seif.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Machi 9, 2019 na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Joran Bashange wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za wabunge wa CUF upande wa Maalim Seif jijini Dar es Salaam na kumtaka Profesa Lipumba na genge lake wajitafakari upya kusuka ama kunyoa.

Bashange amesema kuna mikakati inafanywa ya kumuengua Maalim Seif kinyume na katiba, “njama hizo zinaendeshwa kwa mashinikizo makubwa ya dola kupitia taasisi ya msajili wa vyama vya siasa kwa ufadhili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar lengo likiwa ni kuisambaratisha CUF.”

“Sasa tunasema inatosha na hatutakuwa tayari kuona mkutano huo ukifanyika na tunawaonya wajumbe feki wa mkutano huo waliopanga kuja Dar es Salaam wasije," amesema.

Amesema chama kinatoa wito na tahadhari kwa wote wanaojiita wajumbe wa mkutano mkuu feki wa Profesa Lipumba wasije na wala wasikanyage Dar es Salaam na kwamba Lipumba na genge lake watafakari upya kusuka ama  kunyoa.

“Wasomi na mawakili wa chama wako katika hali ya tahadhari kuchukua hatua endapo itabidi kufanya hivyo,” amesema.

"Wanachama wote wa CUF hapa jijini na walinzi wote watafanya kila liwezekanalo  kuhakikisha wanalinda chama kwa gharama yoyote na hatutasita kuwazuia wanachama wetu kuchukua hatua zozote kadri watakavyoona inafaa ili kuzuia upuuzi huu," amesema.

"Kwa hakika dunia imeshuhudia ustaarabu na uvumilivu wetu kwa kiasi cha kutosha, sasa tunasema inatosha, inatosha. Tunasema inatosha. Sasa basi," amesema Bashange.

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz