MGOMBEA urais Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) Mussa Haji Kombo leo anatarajiwa kuchukuwa fomu kuomba Tume ya uchaguzi Zanzibar (NEC) imteue agombee nafasi hiyo.
Aidha, uongozi wa chama hicho umelaani kauli za mgombea wa urais Zanzibar kupitia chama cha ACT-Wazalendo zenye muelekeo wa kuhamasisha vurugu za kisiasa wakati huu wa maandalizi kwa Uchaguzi Mkuu.
Kombo aliwaeleza waandishi wa habari mjini Unguja kuwa, wataingia katika kinyanganyiro cha urais Zanzibar wakiahidi kulinda amani na utulivu wa nchi na kuepuka vurugu zinazoweza kusababisha wananchi kuishi katika maisha ya dhiki.
''Ndugu waandishi wa habari natangaza rasmi leo nakusudia kuchukuwa fomu kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF...wapo watu walikuwa wakisema kwamba tumeyumba si kweli bado tupo imara” alisema Kombo.
Kombo ni miongoni mwa waanzilishi wa chama cha CUF. Alitaka wananchi wapuuze kauli za Maalim Seif za kutaka vijana wakae tayari kukabiliana na dola kwa kile alichodai vitendo vya uonevu kwa wagombea wa chama hicho kuwekewa pingamizi katika majimbo ya uchaguzi Pemba.
Alisema wananchi Pemba hawajasahau watu waliopoteza maisha kwa sababu za vurugu za kisiasa mwaka 2001 na wengine kuwa wakimbizi Mombasa Kenya.
Alidai kuwa, kwa kiasi kikubwa zilisababishwa na Maalim Seif kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu.
Alisema, kuwekewa pingamizi si jambo jipya kwa kuwa chama hicho kiliwahi kuwekewa pingamizi na chama cha NCCR Mageuzi na kupoteza majimbo sita Pemba lakini hakukuwa na kauli za aina hiyo zinazoashiria vurugu za kisiasa.
“Kauli zilizotolewa na mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad ni za hatari sana zenye kushawishi vijana kuingia katika vurugu za kisiasa eti kwa sababu tu wagombea wa chama chake wamewekewa pingamizi huko Pemba''alisema Kombo.
Alitoa wito kwa mamlaka mbalimbali akiwemo Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuzifanyia kazi kauli hizo kwa kuwa zikiachwa zinaweza kuathiri maendeleo ya uchaguzi kwa kuwatisha wananchi.
“Tunamuomba msajili wa vyama vya siasa ambaye alishuhudia tamko la maadili la vyama vya siasa hivi karibuni kuchukuwa hatua za kisheria kwa ajili ya kukomesha kauli kama hizo ambazo ni hatari kuelekea uchaguzi mkuu” alisema Kombo.
Mgombea Mwenza wa nafasi ya urais wa Tanzania kupitia CUF Hamida Abdallah aliwataka wananchi wakiwemo akina mama kupuuza matamshi ya Maalim Seif kwa madai kuwa mwanasiasa huyo amechoka akili.
Hivi karibuni Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) UV-CCM ulilaani kauli zinazodaiwa kutolewa na Maalim Seif. Kwa mujibu wa UV-CCM kauli hizo zinaashiria uvunjifu wa amani wakati.
Naibu Katibu MNkuu UVCCM, Mussa Haki Mussa aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kauli zilizotolewa na mgombea huo zina lengo la kuwatia hofu wananchi waasijitokeze kupiga kura hazikubaliki.
Musa alisema malalamiko ya kiongozi huyo kuwa baadhi ya wagombea wa ubunge wa ACT-Wazalendo wamewekewa pingamizi na vyama vingine vya siasa hayana msingi.
"Suala la wagombea kuwekewa pingamizi lipo kisheria kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi kifungu namba 51 cha sheria za uchaguzi namba 4 ya mwaka 2008 mgombea aliywekewa pingamizi anayio fursa ya kukata rufaa.