Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF kwazidi kuchafuka, Prof Lipumba atimua vigogo wengine

Lipumbaaapic Data CUF kwazidi kuchafuka, Prof Lipumba atimua vigogo wengine

Sat, 4 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mambo si shwari ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) baada ya mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba kuvunja kamati tendaji Wilaya ya Kinondoni kwa madai ya kuwatukana viongozi wa juu kwenye mitandao ya kijamii.

Hatua hiyo imechukuliwa ukiwa umepita mwezi mmoja tangu chama hicho kilipowatimua na kuwasimamisha uongozi baadhi ya makada wake waandamizi kwa madai ya usaliti.

Hata hivyo, makada hao walikata rufaa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa iliyokipa siku nane chama hicho kutoa maelezo ya hatua kilizochukua.

Kabla sakata hilo halijakauka, juzi Profesa Lipumba aliitisha kikao cha dharura makao makuu Buguruni jijini Dar es Salaam na kuvunja kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 15.

Katika kikao hicho cha dharura kilichodumu saa tatu kikianza saa 12:00 adhuhuri hadi 3:00 alasiri, mwenyekiti huyo wa chama alieleza kuwa amefanya uamuzi huo ili kusimamia nidhamu ndani ya chama hicho.

Hata hivyo, wajumbe wa kamati iliyovunjwa wameeleza huo ni mwendelezo wa ubabe unaofanywa na Profesa Lipumba kuingilia uamuzi uliofanywa na kamati iliyopewa mamlaka na katiba ya chama hicho.

Advertisement Naye Katibu Mkuu wa CUF, Mohammed Ngulangwa alisema uamuzi huo umefanyika kwa kuzingatia katiba ya chama hicho kipengele namba 86 kinachoielekeza kamati ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kufanya hivyo endapo itajiridhisha kamati tendaji ya wilaya imeshindwa kufanya kazi za chama.

Akizungumza na Mwananchi, aliyekuwa mjumbe wa kamati iliyovunjwa ya Kinondoni, Juma Mahimbo alisema licha ya Profesa Lipumba kuivunja kamati hiyo hajawatendea haki, kwani walipaswa kuitwa na kusikilizwa au kujitetea kulingana na tuhuma walizoelekezewa.

“Kamati ambayo mimi ni mmoja wake juzi tulifanya kikao, katika mambo tuliyofanya ni kumsimamisha mwenyekiti wa Wilaya ya Kinondoni, Rajabu Salum kutokana na vitendo vya kuwatukana baadhi ya wajumbe kwenye mitandao na tunaruhusiwa kufanya hivyo na hatuhojiwi,” alisema Mahimbo.

Alisema baada ya kumalizika kwa kikao hicho jana, waliitwa na mwenyekiti wa chama hicho na kuwaeleza kuna kikao cha dharura na ajenda zilikuwa mbili, kwanza kuwapa taarifa ya kuvunja kamati na kuzungumzia mabaya ya ayekuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma, Abdul Kambaya.

Mahimbo alisema Kambaya anatajwa zaidi na Profesa Lipumba akiamini uamuzi uliochukuliwa na kamati ya Kinondoni aliushinikiza, licha ya kufukuzwa kwenye chama hicho kwa makosa mbalimbali.

Alisema kwa kuwa uamuzi uliochukuliwa hawajaridhishwa nao, wanakwenda kuutafakari kabla ya kutoa tamko la pamoja kueleza masuala yaliyopo nyuma ya pazi.

Kwa upande wake, Ngulangwa alisema wanatarajia kutangaza majina ya wajumbe watakaokaimu nafasi hizo hadi mwakani utakapofanyika uchaguzi rasmi kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Kama uamuzi wa kuvunja kamati umefanyika leo (jana) tunatarajia kesho (leo) kamati tendaji itakuwa imepatikana na kikubwa tutajiridhisha kwa wale wanaotakiwa ili tusiwe na mwendelezo wa kuvunja kamati,” alisema Ngulangwa.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz