Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF Lipumba yaungana na Chadema kulia faulo uteuzi Korogwe vijijini

13373 LIPUMBA+PIC TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimeshangazwa na nguvu inayotumika kuwazuia wapinzani kushiriki uchaguzi katika Jimbo la Korogwe Vijijini, licha ya eneo hilo kuwa ngome ya CCM.

Mkurugenzi wa habari na mawasiliano kwa umma wa CUF, Abdul Kambaya alidai kitendo cha wapinzani kuzuiwa kurudisha fomu katika jimbo hilo ambalo mbunge aliyepita alikuwa anakubalika, ni wazi Serikali haijiamini.

Hoja za Kambaya kulalamikia uchaguzi huo pia zimekuwa zikitolewa na viongozi wa Chadema.

Kambaya ambaye yupo upande wa CUF inayoongozwa na mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema CCM ina nguvu katika jimbo hilo.

Alisema CUF inapinga kauli ya mkurugenzi wa uchaguzi, Dk Athuman Kihamia kuwa wagombea wa upinzani walirejesha fomu katika ofisi zisizo sahihi.

Akihojiwa kuhusu sakata hilo kupitia televisheni ya Taifa (TBC), Dk Kihamia alisema hatua hiyo imesababisha mgombea wa CCM kupita bila kupingwa.

Kambaya alisema kauli ya mkurugenzi inatia aibu na kuichafua Serikali kwa kuwa wapinzani walirudisha fomu katika ofisi walikokabidhiwa. Alidai mgombea huyo alipitishwa kinyemela na msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo, Dk George Nyarogwa.

Alisema saa sita mchana Agosti 20 wagombea kupitia vyama vyote akiwamo wa CUF, Kiboko Salehe walifika ofisi hizo kurejesha fomu lakini hawakumkuta mkurugenzi.

“Kauli hii ni ya aibu, wanatoa majibu rahisi katika maswali magumu, kama Serikali haitaki uchaguzi turudi kwenye mfumo wa chama kimoja,” alisema.

Naye naibu mkurugenzi wa ulinzi wa CUF, Masoud Omari ambaye alikuwapo siku ya kurejesha fomu alisema walikuwa pamoja na mgombea wa CCM hivyo wanashangaa kuambiwa wao walikuwa sehemu isiyo sahihi.

“Kilichofanyika ni kitu cha ajabu yaani wagombea wote walikuwa pale hadi wa CCM akiwa na fomu yake, lakini yeye (wa CCM) akarudisha halafu siye tunaambiwa tumepotea ofisi.

“Ghafla, mgombea wa CCM akapewa kama kichumba cha kupumzika kumbe huko ndiko alikopeleka fomu yake, sisi tulisubiri hadi saa 11:00 jioni ndipo alipokuja OCD (mkuu wa polisi wilaya) kutuhoji sababu za kuwapo kwetu ofisi ya Serikali wakati muda wa kazi umekwisha,” alisema.

Omari ambaye pia ni diwani wa Mabanda wilayani Handeni, alisema alishangazwa na figisu hizo na kueleza kama Serikali ilikuwa haitaki uchaguzi kwa nini ilipokea Sh500,000 za kuchukua fomu.

Chanzo: mwananchi.co.tz