Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF Lipumba yapata viongozi wapya Handeni

Sat, 29 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Handeni. Chama Cha Wananchi (CUF) halmashauri ya Mji Handeni mkoani Tanga kinachomuunga mkono mwenyekiti wake anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kimepata uongozi mpya baada ya kufanya uchaguzi  uliofanyika leo Jumamosi Desemba 29, 2018.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi Yusuph Mbungiro ambaye ni ofisa Mafunzo wa CUF Taifa, amesema uchaguzi huo ni wa kawaida kama katiba yao inavyoonyesha kuwa watafanya hivyo kila baada ya miaka mitano.

Katika uchaguzi huo, Awadh Chanyendo alipata kura 113 kati ya kura 129 zilizopigwa ambapo mgombea mwenzake Yusuph Kimicha alipata kura 11 huku kura 2 zikiharibika hivyo Awadh kutangazwa mwenyekiti mpya wa CUF jimbo la Handeni mjini.

Aidha katika uchaguzi huo Masoud Mhina na Jamila Bakari walichaguliwa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu taifa kutoka jimbo la Handeni mjini kinyang’anyiro ambacho kilishirikisha wagombea watano.

Wajumbe wa mkutano huo waliwachagua wajumbe 15 ambao ndio watakuwa wajumbe wa kamati tendaji ya jimbo hilo ambayo inajumuisha wanaume 10 na wanawake watano.

Awadh Chanyendo aliyeshinda nafasi ya mwenyekiti amesema anawashukuru wajumbe kwa kumchagua na kuwataka wanachama wenzake kumpa ushirikiano na kuacha kuwekeana kinyongo wenyewe kwa wenyewe.

Mjumbe wa mkutano mkuu taifa, Mhina amesema wanachama wasiwe na wasiwasi wao kama viongozi watahakikisha wanaondoa tofauti na kujenga CUF moja yenye nguvu.

“Tutahakikisha kuwa CUF inakuwa imara na tuna uhakika wa kufanya vizuri kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa mpaka ubunge na wote tuwe kitu kimoja ili kufanikisha  haya,” amesema Masoud.

Mmoja wa wajumbe katika uchaguzi huo Issa Mkala amesema viongozi hao wahakikishe wanaondoa mivutano katika chama kwani madhara yamekuwa makubwa kwa wanachama kuyumba kundi moja kumuunga mkono Profesa Lipumba na wengine Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.



Chanzo: mwananchi.co.tz