Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CUF, ACT 'zinavyoupiga mwingi' Zanzibar

Cufpic Chama cha Wananchi CUF

Thu, 24 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kati ya mwaka 1992 mpaka 2019, siasa za upinzani Zanzibar zilijengwa kuzunguka chama kimoja, Civic United Front (CUF). Kutoka mwaka 2019 hadi sasa, kinara wa upinzani visiwani ni Alliance for Change and Transparency-Wazalendo (ACT-Wazalendo).

Kutoka mwishoni mwa miaka 1980, ujio wa siasa za vyama vingi vya siasa mwaka 1992 hadi Februari 17, 2021, siasa za upinzani Zanzibar zilijengwa kumzunguka mwanasiasa mmoja, Seif Sharif Hamad ‘Maalim Seif’.

Kipindi CUF wakiongoza mwendo wa upinzani Zanzibar, mhusika mkuu alikuwa Seif na ACT-Wazalendo walipochukua kijiti kama alama kuu ya siasa za mageuzi Zanzibar, kinara alikuwa Seif.

Machi 18, 2019, Seif alipotangaza kuhama CUF na kujiunga na ACT-Wazalendo, viongozi wengi waliokuwa CUF na wanachama, walihama naye. Hata wabunge waliokuwa CUF, wote mara Bunge lilipovunjwa, walihamia ACT.

Mantiki ambayo haibishaniwi na haijawahi kubishaniwa popote ni kuhusu nani alifuatwa. Wote wanakubali kuwa aliyesababisha wimbi kubwa liondoke CUF na kujiunga na ACT-Wazalendo ni Seif.

Sasa, Seif ameshaondoka. Inaelezwa kuwa wanachama zaidi ya 100 wamerejea CUF. Ni baada ya uchaguzi wa ndani wa ACT-Wazalendo, kujaza nafasi ya Mwenyekiti, iliyoachwa wazi na Seif. Suala la kuhama chama baada ya uchaguzi wa ndani ni kawaida. CUF yenye Prof Ibrahim Lipumba na Maalim Seif, iliwapoteza wanachama wengi, wakiwemo viongozi wa ngazi za juu kabisa. Prof Abdallah Safari alihamia Chadema kutoka. Wilfred Lwakatare alihamia Chadema pia. Hawa walikuwa viongozi waandamizi.

Safari na Lwakatare ni mfano mdogo kuonyesha kuwa baada ya uchaguzi wa ndani, kwa historia ya Tanzania, vyama vya upinzani huwa havibaki salama asilimia 100. Hili la ACT-Wazalendo si jipya kuondokewa na wanachama wake.

Desemba 2019, Chadema waliondokewa na wanachama wao wengi tu, tena waandamizi na waliokuwa viongozi. Walinung’unika kuminywa kwa demokrasia ndani ya chama.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani, Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini, Cecil Mwambe, vilevile Prof Safari, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, walijiondoa kwenye chama hicho. Mwambe na Sumaye walielelea CCM, Safari hajaeleweka.

Uchaguzi wa ndani ACT-Wazalendo mwaka 2020, ulipomalizika kuna ambao walitimka. Mmoja wao ni Jeremiah Maganja, aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo. Maganja alihamia NCCR-Mageuzi, alikosimama kama mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu 2020

Mwaka 2003, Chadema walipofanya uchaguzi, Freeman Mbowe, alipochaguliwa kuwa mwenyekiti kwa mara ya kwanza, kuna kundi la wanachama waandamizi waliondoka. Kikazaliwa chama kingine, Demokrasia Makini.

Hivi karibuni, ACT-Wazalendo, walifanya uchaguzi kujaza nafasi ya mwenyekiti. Juma Duni Haji ‘Babu Duni’ alimshinda Masoud Hamad Masoud. Kisha, Masoud akajiondoa kwenye chama hicho, amekwenda Cuf.

Kuna viongozi wengine wa ACT-Wazalendo, wamekwenda CUF. Wengi wao ni wale waliohamia ACT-Wazalendo kutokea CUF, katika mkumbo wa Seif, isipokuwa Mtumwa Kimwanga, ambaye alijiunga na ACT-Wazalendo tangu mwaka 2015, akitoka kuwa mbunge viti maalum CUF.

Kumbe sasa, hoja sio wanachama kuhama ACT-Wazalendo kwenda CUF baada ya uchaguzi. Hilo ni jambo lililozoeleka kwa vyama vya upinzani Tanzania. Hata akina Mabere Marando waliposhindwa na James Mbatia NCCR-Mageuzi, waliondoka. Marando ni mwasisi wa NCCR-Mageuzi.

Hoja ambayo inapaswa kujengwa hapa ni tafakuri ya jinsi ambavyo siasa za upinzani zitakuwa baada ya huu mwanzo wa kuihama ACT-Wazalendo wakati ambao Maalim Seif ameshalala kwenye tumbo la ardhi.

Machi 2019, wakati Seif alipotambulisha kauli mbiu ya “Shusha Tanga Pandisha Tanga”, aliondoka na vigogo wote wa upinzani katika siasa za Zanzibar waliokuwa CUF. Haguswi Hamad Rashid Mohamed, ambaye alipohama CUF, alikwenda kuanzisha chama kipya, Alliance for Democratic Change (ADC).

Hata sasa, ikiwa ni mwaka mmoja tangu Seif afariki dunia, vigogo wote wa ACT-Wazalendo, waliohamia na Seif bado wapo pamoja. Na wanaendelea kushiriki Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Hamad Rashid bado yupo ADC.

Swali ni je, ACT-Wazalendo wanaweza kuendelea kushikilia siasa za Zanzibar ikiwa wanachama wake wengi wamerejea CUF? Jibu la swali hilo litakuja kwa maelezo kidogo, mifano na maswali ikibidi.

Je, ACT-Wazalendo watetereke Zanzibar halafu CUF waimarike? Kumbuka, sasa hivi CUF wana mgogoro wa uongozi na kesi ipo mahakamani. Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar, Mussa Haji Kombo na wenzake wanamshtaki Prof Lipumba kwa kuwafukuza uanachama.

Kwa mantiki hiyo, hata CUF ambayo inakimbiliwa nako moto unawaka. Hivyo, huoni kama wanachama walioondoka ACT-Wazalendo kwenda CUF, wanaweza kukidhoofisha chama hicho.

Lenye kupaswa kuangaliwa ni uimara wa upinzani baada ya Seif, vilevile ACT-Wazalendo kuendelea kuongoza siasa za mageuzi bila Seif. Kisha, chukua alama za upinzani Zanzibar kwa miaka yote.

Haibishaniwi kuwa siasa za mageuzi Zanzibar zilijikita kwenye jina la Seif. Na hakuna mwanasiasa mwingine yeyote aliyeibukia upinzani Zanzibar, aliyewahi kuthubutu kutikisa msuli wa Seif. Kila aliyejaribu alikwenda na maji.

Hamad Rashid ni mwanasiasa mkongwe na mahiri mno. Alishapata kuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa Zanzibar ana historia ndefu serikalini, kwenye mashirika ya umma na uongozi wa kisiasa. Hata hivyo, alipojaribu kujipima ubavu na Seif, alikwenda na maji.

Majina makubwa mengine ya kisiasa upande wa upinzani Zanzibar, yapo ACT-Wazalendo, na wengi wao ni wale walijipambanua kisiasa kumzunguka Seif. Babu Duni, Nassor Mazrui, Salim Bimani, Jussa Ismail, Mansoor Himid, Othman Masoud, ambaye sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, na wengine, wote wapo ACT-Wazalendo.

Swali ni je, upinzani utaendelea kuwa na nguvu ileile baada ya Seif? Hapo ndipo kwenye kitendawili kizito.

Ikiwa ACT-Wazalendo upande wa Zanzibar wataweza kubaki wamoja na wakasimama na agenda za Seif kunusu visiwa vyao bila kuyumba, bila shaka chama hicho kitaendelea kutetea nguvu ya upinzani dhidi ya CCM.

Kama ACT-Wazalendo watavurugana wao kwa wao, vinara wakagombana na wengine kuhama, sio tu kwamba chama hicho kitapoteza nguvu zake za kisiasa, bali pia kitasababisha upinzani Zanzibar upoteze nguvu zake kabisa. Maana upinzani Zanzibar kwa sasa umejengeka kupitia ACT-Wazalendo.

Cuf bado ipo kwenye migogoro na haionekani kunyanyuka imara hivi karibuni. ADC, mpaka sasa hakijaonesha uimara wowote Zanzibar. Zaidi kinaonekana ni sura ya mtu mmoja, Hamad Rashid ambaye hana jeuri kwa sasa kushindana na miamba ya kisiasa iliyopo ACT-Wazalendo.

Watu kama Jussa na Othman walikuwa vijana wadogo kipindi Hamad Rashid na wengine, wakichora mstari wa kudai haki za Wazanzibari mwanzoni mwa miaka ya 1990. Hata hivyo, siku ni wanasiasa wakubwa na wanatazamwa kuliko Hamad, hapo hujawataja Duni, Bimani, Mazrui, Himid na wengine.

Uimara wa upinzani Zanzibar utaendelea kutegemea jinsi ambavyo ACT-Wazalendo watabaki wamoja na watakavyosimama imara. Watu wanao na thamani zao zilijengwa vizuri na Seif. Chama hicho kikitetereka, haitakuwa sababu ya chama kingine kunyanyuka, bali CCM watazidi kutamalaki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live