Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA yavijibu tena Vyama 14 Ripoti ya Kikosi Kazi

Chademapic 600x400 CHADEMA yavijibu tena Vyama 14 Ripoti ya Kikosi Kazi

Sat, 29 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema njaa iliyopitiliza, kutumika na kukosa dira ya masuala ya kitaifa ni sababu ya baadhi ya vyama vya upinzani kupinga msimamo uliotolewa na chama hicho juu ya ripoti ya Kikosi Kazi.

Oktoba 23 mwaka huu, muungano wa vyama 14 vya upinzani ulitoa tamko la kulaani na kujitenga na msimamo uliotolewa na Chadema inayodai hakukuwa na umuhimu wa kuundwa kwa Kikosi Kazi cha kukusanya maoni kutafuta muafaka wa kitaifa uliotokana na mkwamo wa kisiasa.

Msimamo huo unaoendelea kuleta sintofahamu ndani ya vyama vya upinzani nchini kiasi cha kutofautiana kimtazamo na kuacha chama tawala kikijiweka kando, ulianza siku mbili baada ya Kikosi Kazi kukabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Umoja huo unaundwa na vyama vya ADC, NCCR-Magezi, TLP, Demokrasia Makini, Tadea, NRA, Sauti ya Umma, SAU, UPDP, NLD,AFP, CCK, UDP, DP na UMD.

Jana, umoja wa wenyeviti 10 wa majimbo ya Chadema, Dar es Salaam ulizungumza na waandishi wa habari ukisema vyama hivyo vinatumika vibaya na vikipewa nafasi vitavuruga msimamo na dhamira ya Watanzania kupata mageuzi.

“Hata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, vyama hivyo vilipata kura chache sana chini ya asilimia 0.2 na ukipiga kura za vyama vyote haviwezi kufikia hata nusu ya kura ambazo Chadema walipigiwa kura na Watanzania,” alisema Mwenyekiti wa Jimbo la Kawe, Leonard Manyama.

Mwenyekiti wa Jimbo la Kibamba, Ernest Stanley alisema Watanzania wanapaswa kupuuza matamko yanayotolewa na muungano huo.

“Vyama hivyo vinakusanyana na kuishambulia Chadema; na hata kwenye mikutano yao wanasoma andiko ambalo wameandikiwa yote hayo kutaka kuipinga Chadema, Watanzania wapinge kwani vinataka kurudisha nyuma ustawi wa demokrasia,” alisema Staniley.

Mwenyekiti wa Jimbo la Ukonga, Sweya Omary alisema vyama hivyo havijakomaa kisiasa na wanajikuta wakitumika bila kujua malengo ya kuundwa kwa vyama vyao ni kuwakomboa Watanzania.

Akijibu hoja hizo za Chadema, kwa niaba ya muungano wa vyama 14 vya upinzania nchini, Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo alisema kuwatuhumu wao wanatumika ni lugha tu ya watu waliokosa kujibu hoja iliyojengwa.

“Sisi upande wetu hatuzungumzii chama chochote kutumika, tunawapinga wao, jambo ambalo hawajashiriki wanaona si sahihi, yaani tuwasubiri Chadema watakapoanza kushiriki tuseme sawa kwa masilahi ya Taifa, hatuwezi kwenda hivyo kama mbuzi wa kuchungwa,” alisema Doyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live