Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA yasema haija lala, mapambano yanaendelea

Chademapic Kutoshiriki CHADEMA yasema haija lala, mapambano yanaendelea

Tue, 15 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema chama hicho kinazungumza na Serikali lakini mazungumzo hayo hayazuii mapambano yao kutaka haki na ahueni kwa raia.

Tangu Mei, Chadema kilianza kuzungumza na Serikali pamoja na viongozi wa juu wa CCM kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo kushughulikiwa kwa madhara yaliyotokana na ukiukwaji wa haki uliofanywa katika kipindi cha miaka sita ya utawala wa Serikali ya awamu ya tano.

Suala jingine ni kupatikana kwa Katiba Mpya, Chadema wakipendekeza hatua za kupitia, miundo ya vyombo vinavyohitajika ili kuharakisha mchakato na muda utakaotumika kuikamilisha kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Wakati mazungumzo hayo yakiendelea, Mnyika akiwa wilayani Masasi mkoani Mtwara jana katika ziara yake alisema chama hicho hakitochoka kuzungumzia changamoto na kero za wananchi.

Mnyika alisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi wa mikoa ya kusini ni mwenendo usioridhisha wa bei ya korosho, suala la gesi pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama tatizo ambalo pia limeikumba mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Pwani kutokana na ukame uliopo hivi sasa.

“Licha ya mazungumzo kuendelea, hatutaacha kusema kwa sababu ya kusubiri Katiba Mpya au mazungumzo yetu. Hatuwezi kuyaacha matatizo ya wananchi pembeni kwa sababu hatima ya kusini sio kwa wananchi mikoa hii tu bali ni ya Taifa zima,” alisema.

Alisema Chadema kipo pamoja na wananchi wa mikoa ya kusini na kitaendelea kuwasemea changamoto zao na akawataka kuandika barua itakayoanisha matatizo yao ili kuyafikisha kwa watawala kuhusu bei ndogo ya korosho na kukosekana kwa maji safi.

“Zungumzeni kwa lugha ya watu wa kusini itakayoeleweka, semeni na msichoke ili watawala wasikie kilio kuhusu bei, maji na korosho. Jukumu lenu sasa ni kufanya mambo matatu ili nguvu isiwe ya leo tukitoka hapa ihamie kwenye kata, matawi, hata majimbo na mikoa ya jirani.Nguvu ya kusini ikiendelea hivi sauti za changamoto zenu zitawafikia tunataka iwe sauti ya korosho, endeleeni kutumia nguvu ya kusini,” alisema.

Mnyika alisema lengo la Chadema kuiweka Katiba Mpya kama kipaumbele ni kulinda haki za watu kwa sababu ni uhai wa watu na Taifa kwa ujumla.

Awali, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mtwara, Shaban Mbarouk alisema chama hicho kimepitia mengi lakini sasa ni wakati wa kusonga mbele. Alisema Chadema ndiyo chama kinachoweza kuwatetea wananchi kwa changamoto zote zinazowakabili.

“Katibu mkuu ukweli bado korosho inatuumiza, tushirikiane kupaza sauti ili kuwasaidia wananchi wa Mtwara na Lindi. Jambo jingine siasa ni mikutano, pamoja na maridhiano yanayoendelea lakini tunaomba ufikishe salamu kwa Rais Samia afungue mikutano ya hadhara ili shughuli za siasa ziendeleea,” alisema Mbarouk.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kusini, General Kaduma alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili Katiba Mpya, tume huru na maandalizi ya uchaguzi wa ndani ya chama hicho na kuwasisitiza wanachama kujisajili kidijitali.

Alisema lengo jingine ni kukiimarisha chama hicho, akisema Mnyika atakuwa mkoani Lindi akizungumza na wanachama wa chama hicho.

Wiki mbili zilizopita Mnyika alikuwa na ziara katika kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Iringa ambako alikutana na viongozi na wanachama kuweka mikakati ya kuendesha siasa zao.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live