Siku tatu baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro kueleza kuwa jeshi hilo litaanza kuchunguza mitalaa ya mafunzo yanayotolewa katika vyuo na shule za dini, Chadema imesema kiongozi huyo wa polisi amevunja sheria na katiba ya nchi.
Septemba 11, IGP Sirro baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Rwanda, alisema hatua ya kuchunguza mitalaa ya vyuo na shule zinazomilikiwa na taasisi za dini ni njia ya kupambana na makosa ya kigaidi na kuhakikisha shule na vyuo vinavyomilikiwa na taasisi hizo zinawafundisha watoto uzalendo.
Akizungumza na vyombo vya habari jana mkoani Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema –Bara, Benson Kigaila alisema hatua hiyo ya IGP Sirro ni kuingilia uhuru wa taasisi za dini, jambo alilodai ni uvunjifu wa Katiba. Alinukuu ibara ya 19(3) ya Katiba ya nchi inayoeleza, “Katika kueneza dini au kuendesha ibada, mamlaka ya kuendesha ibada hizo haitaingiliwa na mamlaka za Serikali.” “Tunahitaji Katiba itakayotoa adhabu moja kwa moja pale uvunjifu wa sheria unapotokea na kuupatia suluhisho, uzalendo si kuvumilia uvunjifu wa amani,” amesema Kigaila
Hata hivyo, juhudi za kumpata IGP Sirro ili afafanue suala hilo zilishindikana na alipotafutwa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alifafanua suala hilo kwa kusema hii si mara ya kwanza kufuatilia maeneo hayo. Alisema: “Nani asiyejua malalamiko yalishawahi kutolewa kuhusu baadhi ya nyumba za ibada kutumika kwa mazoezi usiku na ufuatiliaji ukafanyika,” alisena na kuongeza:
“Pia, malalamiko yamewahi kutolewa kuwa baadhi ya nyumba za ibada kuna ibada zinaendelea usiku wa manane na kusababisha usumbufu kwa wengine,” alisema Misime.
Aliongeza kuwa kuna malalamiko ya watoto wadogo walioonekana wamekusanywa katika nyumba fulani, ilipofuatiliwa ilibainika mazingira walimokuwa wakifundishwa dini hayafai na hawakuwa wamefikia umri wa kutenganishwa na wazazi wao.