Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza nia yake ya kulitwaa Jimbo la Chato kwa kushinda viti vingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na ule wa ubunge na madiwani mwakani.
Jimbo hilo ambalo kwa muda mrefu tangu likiwa Biharamulo Magharibi mwaka 1995 hadi lilipoitwa Chato baada ya kuanzishwa wilaya, lilikuwa chini ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dk. John Magufuli mpaka mwaka 2015 na baada ya hapo Dk. Medard Kalemani mpaka sasa. Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria, Hezekiah Wenje, ambaye anawania tena nafasi hiyo, amesema kuwa Chato ni moja ya majimbo yaliyoko katika kanda hiyo ambayo wamepania kushinda yote katika uchaguzi ujao.
"Kwa kanda nzima ya Victoria katika majimbo 25, mpango wetu ni kupata majimbo si chini ya 16 likiwamo la Chato na uwezekano upo. Tumeshafanya tathmini na utafiti wa kutosha.
"Kwa mfano Jimbo la Chato tumewahi kuongoza serikali za vijiji vingi kuliko Chama Cha Mapinduzi (CCM) tena kipindi cha Magufuli," amesema. Wenje amesema hiyo ni miongoni mwa mikakati yake endapo atateuliwa tena kugombea kanda hiyo na kuitetea kwa mara nyingine.
Kamati Kuu ya CHADEMA iliyoketi Dar es Salaam tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, ilihitimisha vikao vyake jana ambavyo pamoja na mambo mengine, ilifanya usaili wa wanaoomba nafasi za uongozi katika kanda.
Katika hatua nyingine, baadhi ya viongozi wa CHADEMA wameeleza matumizi ya jengo jipya la ofisi za chama hicho, Mikocheni, Dar es Salaam, yalivyopunguza gharama ambazo zingetumika katika kikao cha kamati kuu. Kwa mara ya kwanza, chama hicho kilitumia jengo hilo ambalo kilinunua tangu mwaka jana.
Mara kadhaa, chama hicho kinapokuwa na vikao vya kamati kuu, kilikuwa kikijichimbia kwenye hoteli za kifahari katika mikoa mbalimbali, hasa Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Itifaki na Mawasiliano kwa Umma, John Mrema, amesema kwa kutumia ofisi hiyo mpya, kuna gharama kubwa wameokoa lakini pia wamepata utulivu mzuri wa kujadili hoja mbalimbali.
"Ni kweli kuna gharama zinapungua. Ukikaa kwenye hoteli huko ukichukua mkataba wanakwambia mpaka saa fulani mwisho lakini ukikaa hapa hata tukimaliza saa 7:00 usiku hakuna mtu wa kutubughudhi.
“Baada ya kumaliza kikao hiki tutakaa tupige hesabu zilizotumika hapa halafu tulinganishe na zile ambazo tumekuwa tukitumia kwenye vikao kama hivi tukifanyia hotelini," amesema.
Frank Mwakajoka anayetia nia katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti Kanda ya Nyasa, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Tunduma, amesema wazo la kufanyia vikao katika ofisi hizo ni jema kwa sababu wanaamini kwamba fedha iliyookolewa kwa kutokufanyia katika hotelini ni kubwa na itafanya kazi zingine za chama.
Naye Ezekiel amesema: “Ni salama zaidi na imepunguza gharama kwa kiasi kikubwa. "Kwa akili ya kawaida tu ni lazima gharama zimepungua tena nyinyi. Mnajua viwango vyetu tulikuwa tukikodi ukumbi mara Bahari Beach mara wapi lakini sasa tuko katika ofisi zetu.
"Hata kiusalama pia ni uhakika kwa sababu haya ni majengo yetu hatuna wasiwasi kwamba mtu anaweza kukuwekea kakitu kwa chini hivi na tuna CCTV camera za kwetu kwa hiyo hakuna wasiwasi."