Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA yaitaka Serikali kutoa majibu kupanda bei za vyakula

MNYIKA123 CHADEMA yaitaka Serikali kutoa majibu kupanda bei za vyakula

Mon, 17 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeitaka Serikali kutoa kauli rasmi nje ya Bunge na ndani ya Bunge kueleza mkakati wa kuwezesha kushuka kwa bei ya vyakula na kueliepusha taifa balaa la njaa kutokana na kuwepo kwa viashirio vya upungufu wa chakula katika miezi michache ijayo.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika, wakati akifunga mafunzo ya mawakala watakaotumika kusajili wanachama kupitia mfumo wa Kidigitali unaoanza rasmi katika majimbo matatu ya Morogoro, Kilombero na Mlimba mkoani Morogoro.

Mnyika amesema wakati Taifa likiadhimisha siku ya chakula Duniani watanzania wanalia na hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa bei ya chakula huku Serikali ikikaa kimya.

“Leo ikiwa ni siku ya chakula duniani na tupo katika mkoa ambao umebarikiwa na mwenyezi Mungu kuwa katika mkoa wenye rutuba na maji na mkoa wenye uzalishaji wa chakula katika nchi yetu, lakini Watanzania wanalia na hali ngumu ya maisha kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula, hivyo tunaitaka serikali kutoa kauli yake jinsi ya kupunguza bei ya vyakula” amesema Mnyika.

Katibu huyo Mkuu wa Chadema amesema pamoja na kupanda kwa bei ya vyakula lakini ipo hatari mbele ya upungufu wa chakula nchini kwa baadhi ya mikoa hivyo ni lazima Serikali ikatoa kauli au kueleza mikakati kwa wananchi ya kukabiliana na hali hiyo.

Amesema Serikali isisubiri hasira za wananchi zikazidi kuongezeka kwakuwa njaa ikizidi au gharama za vyakula zinavyozidi kupanda, Chadema haitaweza kushiriki kudhibiti hizo hasira za wananchi.

Akizungumzia kuhusu Bima ya afya kwa wote, Mnyika amesema tayari maoni yanakusanywa na mwezi Novemba muswaada wa bima utawasilishwa kwenye Bunge na kwamba tayari Kamati kuu ya Chadema imeshatoa kauli kuwa usisomwe kwa hati ya dharura usomwe kwa hati ya kawaida ili kutoa nafasi kwa wananchi wauone.

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa Chadema alimupomba Rais Samia Suluhu Hassani kutimiza ahadi yake ya kuruhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa aliyoitoa siku ya Demokrasia ya Vyama vingi.

Awali Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Morogoro, Jackson Malisa alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kusimamisha msafara wa Katibu Mkuu wa Chadema ni aibu kwakuwa tayari kuna majadiliano yanaendelea kuhusu vyama vya siasa kufanya kazi zake bila kuingiliwa na jeshi hilo.

Naye Mwenyeti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Devota Minja alisema mafunzo hayo kwa mawakala yamelenga kusajili wanachama nyumba kwa nyumba katika majimbo hayo matatu kuingizawa katika mfumo wa kidigitali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live