Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA yagomea tena chaguzi ndogo

Chademapic Kutoshiriki CHADEMA yagomea tena chaguzi ndogo

Tue, 22 Nov 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimegomea chaguzi ndogo zitakazofanyika Desemba 17, 2022 katika maeneo mbalimbali nchini huku ikitishia kususia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu 2025.

 Chadema imekwenda mbali zaidi ikisisitiza kwenye chaguzi za 2024 na ule wa 2025 kama hakutakuwa na mabadiliko ya katiba, imetishia chaguzi hizo kutofanyika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Novemba 22, 2022, makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Bara, Singo Kigaila amesema msimamo wa chama hicho ni kutoshiriki chaguzi zote ndogo kipindi hiki.

“Tumepokea taarifa ya tume kuwa na uchaguzi wa jimbo la Amani, Zanzibar na kata 12 za Halmashauri mbalimbali za bara, kama chama msimamo wetu huko pale pale hatutoshiriki," amesema.

Kata hizo ni ya Njombe Mjini (Mji Njombe), Misugusugu (Kibaha), Lukozi (Lushoto), Mndumbwe (Tandahimba), Dabalo (Chamwino), Kalumbaleza (Sumbawanga), Ibanda (Kyela), Dunda (Bagamoyo), Mnyanjani (Tanga), Mwamalili (Shinyanga), Vibaoni (Handeni) na Majohe, Dar es Salaam.

"Kwenye chaguzi hizi, msimamo wa chama ni kwamba hatushiriki, hatuwezi kushiriki kwenye 'maigizo'," amesema.

Akifafanua 2024 na 2025, amesema wako kwenye majadiliano na Serikali ya kutaka uwepo wa katiba mpya ambayo itazaa tume huru ya uchaguzi, sheria na muundo bora wa uchaguzi.

"Kama hivyo havitafanyika, basi hata huo uchaguzi wenyewe hautofanyika," amesema.

Kuhusu majadiliano na Serikali, amesema kuna kamati ya maridhiano inaendelea na mazungumzo.

Hata hivyo, amevishauri vyama vingine vya upinzani kuungana nao katika kudai katiba mpya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live