Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA yafunguka kuhusu ruzuku

Mnyikaaaa CHADEMA yafunguka kuhusu ruzuku

Mon, 3 May 2021 Chanzo: ippmedia.com

Akizungumza na Nipashe, Katibu Mkuu wa CHADEMA taifa, John Mnyika, alisema viti maalum havichangii lolote kwenye ruzuku ya chama chochote cha siasa.

“Hadi sasa hatujapokea fedha yoyote kutoka Hazina wala Msajili wa Vyama vya Siasa kama inavyoelezwa… ni kama propaganda inafanyika kulazimisha kuwa viti maalum ndiyo vitaleta ruzuku kwenye chama,” alisema Mnyika.

Alisema kumekuwa na upotoshaji mkubwa kuwa wabunge 19 ambao walishafukuzwa na chama hicho ndiyo watasaidia chama kipate ruzuku, na kwamba kikokotoo cha zuruku hakitumii wabunge wa viti maalum.

Alisema ruzuku hupatikana kwa idadi ya kura za ubunge kuanzia asilimia tano kuendelea na kiti cha ubunge wa jimbo katika uchaguzi mkuu.

“Ruzuku inayotajwa ya Sh. milioni 109 kama ndiyo, itatokana na kura za wabunge, viti maalum havihusiki kwa namna yoyote ile katika kupewa au kutokupewa ruzuku kwa chama chochote kile,” alisema Mnyika.

Kwa mujibu wa Mnyika, kura za urais nazo hazina msaada wowote katika chama kupata ruzuku na ndiyo maana chama kinaweza kisiwe na mbunge hata mmoja, lakini kikapata ruzuku kutokana na kura za ubunge kuzidi asilimia tano.

Tangu wabunge 19 wa viti maalum kukubali kuapa na kuingia bungeni, kumekuwa na mvutano mkali, ikiwamo mijadala katika jamii.

CHADEMA inasema haijahusika kwa namna yoyote kutoa majina ya wabunge hao na wala hakuna aliyejaziwa fomu na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama kama sheria inavyoelekeza, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilitangaza majina wa wabunge hao na waliapishwa Novemba 24, mwaka 2020 na Spika Job Ndugai.

Novemba 27, mwaka huu, CHADEMA ilitangaza kuwavua nyadhifa zao wabunge hao na kuwafuta uanachama.

Wabunge hao 19 walidai kuwa walikata rufani kwenye Baraza Kuu cha CHADEMA, ambalo hadi sasa halijakutana kupitia rufani hizo.

Katiba ya nchi imetaja aina za wabunge ni wa majimbo, viti maalum ambao lazima watokane na chama cha siasa na viti 10 vya rais.

Wabunge hao 19 wa viti maalum ni Halima Mdee, Grace Tendega, Ester Matiko, Cecilia Pareso, Ester Bulaya na Agnesta Kaiza.

Wengine ni Nusrat Hanje, Jesca Kishoa, Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Felister Njau na Naghenjwa Kaboyoka.

Pia, wamo Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stela Fiayo, Anatropia Theonest, Salome Makamba, Conchesta Rwamlaza na Asia Mohammed.

Chanzo: ippmedia.com