Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA yaanika mikakati kudai Katiba

TunduLissu?fit=800%2C445 Chadema yaanika mikakati kudai Katiba

Mon, 3 Jan 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeazimia kuanza mwaka mpya na mkakati wa kupigania kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba mpya, ambao utawaunganisha wadau mbalimbali.

Pia, chama hicho kimeeleza kwamba hakitashiriki katika shughuli zozote za Baraza la Vyama vya Siasa kwa madai kwamba malengo yake ni kuua na kuzika ndoto za matamanio ya Watanzania kujipatia Katiba mpya.

SOMA: Zitto asema mwaka 2021 ulikuwa na mitihani mikubwa

Chadema imetoa msimamo huo wakati tayari Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ikiwa imeunda kikosi kazi ambacho kitapitia hoja zilizopitishwa kwenye mkutano wa wadau wa demokrasia nchini na kutoa mapendekezo ambayo yatawasilishwa serikalini.

Katika mkutano huo uliofanyika Desemba 16 jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliahidi kwamba mapendekezo yatakayotolewa na wadau wa mkutano huo yatafanyiwa kazi na Serikali yake.

Hata hivyo, katika mkutano huo wa wadau, hoja 81 ziliibuliwa na hoja hizo zitakwenda kuchakatwa na kikosi kazi hicho kisha kutoa mapendekezo yao. Baadhi ya hoja hizo ni pamoja na sheria ya vyama vya siasa na Jeshi la Polisi kufanyiwa marekebisho na vyama kuruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara.

Advertisement Vilevile, waliibua hoja za kuwa mchakato wa Katiba mpya usiendelee, badala yake yaangaliwe mambo machache yanayolalamikiwa na katiba inayopendekezwa ifanyiwe marekebisho na kupitishwa badala ya kuanza mchakato upya.

Lissu na salamu za mwaka mpya

Akizungumza juzi kwa njia ya mtandao wakati akitoa salamu za mwaka mpya, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alisema kwa muda mrefu Katiba imekuwa ikiwekewa viraka, hivyo wao wanatamani kuona mchakato wake ukianzia kwenye rasimu ya Jaji Joseph Warioba.

Alisema Katiba ya sasa ina jumla ya viraka 13 tangu mfumo wa chama kimoja ulipoanzishwa na kwamba kama ingekuwa ni nguo, mtu hawezi kujua kipi ni kitambaa chake cha awali na kipi ni kitambaa cha viraka.

“Sisi wa Chadema tunapendekeza kuanzishwa kwa mchakato wa katiba ya wananchi ambao utaunganisha vyama vya siasa, makundi mbalimbali ya kijamii, taasisi za kidini, taasisi za kitaaluma na asasi zisizo za kiserikali ambazo zinaunga mkono madai ya katiba mpya na rasimu ya Warioba.

“Chadema itapendekeza kwa wale wote watakaoungana nasi katika kudai katiba mpya kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi juu ya rasimu ya Warioba kwa njia ya mikutano ya hadhara na makongamano yatakayofanyika sehemu mbalimbali za nchi yetu,” alisema Lissu.

Kiongozi huyo wa Chadema anayeishi Ubelgiji, alisisitiza kwamba Tanzania haihitaji tena katiba yenye viraka, bali inahitaji katiba mpya inayoendana na mabadiliko na matakwa na hali na mazingira ya sasa.

Lissu alieleza kwamba kamati kuu iliyoketi Desemba 28, imeazimia kuwa Chadema hakitashiriki katika katika shughuli zozote za Baraza la Vyama vya Siasa, kwa madai kwamba malengo yake ni kuua na kuzika ndoto za matamanio ya Watanzania kujipatia katiba mpya.

“Sisi wa Chadema pamoja na NCCR- Mageuzi tulitangaza kutoshiriki kwenye mkutano huo, kwa sababu hapajawahi kuwa na mazingira mwafaka ya kushiriki mikutano au vikao vya aina hiyo,” alisema Lissu.

Alidai kwamba kikosi kazi kilichoundwa kimejaa wanachama wa CCM, hivyo wao hawataki kuwa sehemu ya kikosi hicho ambacho anaamini hakitaleta mabadiliko yanayohitajika.

Lissu, Lema kurejea nchini

Lissu alisema kamati kuu ya Chadema iliazimia kwamba yeye na aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema aliyekimbilia nchini Canada wanatakiwa kuanza maandalizi mapema ya kurejea nchini kati ya Machi na Aprili mwaka huu.

Alisema kamati kuu iliridhia kwamba chama kianze maandalizi ya ujio wao kwa upande wa Tanzania na baada ya maandalizi yote kukamilika, tarehe ya kurudi kwao itatangazwa rasmi kwa wanachama, wafuasi na wapenzi wa Chadema.

Maoni ya wadau

Akizungumzia uamuzi huo wa Chadema, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie alisema Katiba mpya ni ajenda kuu ya Chadema, hivyo hakuna siku wataiondoa ajenda hiyo mpaka pale watakapofanikiwa.

Alisema chama hicho kimeona namna pekee wanayoweza kushiriki katika siasa hapa nchini ni baada ya Katiba mpya, hivyo wanapambana kutengeneza mazingira bora ya kisiasa ambayo wanayahitaji.

“Katiba mpya ni ajenda yao, hata ukifuatilia mazungumzo yao utaona ni Katiba Katiba. Hawawezi kuiacha ajenda hiyo ikaishia hewani, wataisimamia hadi hapo watakapoona wameridhika,” alisema Dk Loisulie.

Kuhusu kurudi kwa wakimbizi wa kisiasa, Dk Loisulie alisema wameona mazingira ya kisiasa ya sasa siyo korofi ukilinganisha na siku za nyuma, hivyo wana uhakika kwamba wao na familia zao watakuwa salama.

Akiwa na mtazamo kama huo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Abdallah Safari alisema hitaji la katiba mpya siyo la Chadema, bali ni la Watanzania wengi, hivyo Chadema wanatakiwa kuungwa mkono katika mapambano hayo.

“Katiba wanayoipigania ni ya Watanzania wote, kwa hiyo wanastahili kuungwa mkono ili kufanikisha mchakato huo,’’ alisema.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz