Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA wazuiwa kuingia gerezani kumwona Mbowe

GEREZA KUU UKONGA 0 CHADEMA wazuiwa kuingia gerezani kumwona Mbowe

Sun, 24 Oct 2021 Chanzo: ippmedia.com

Baadhi ya viongozi wa CHADEMA wamedai kuzuiwa kumuona Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye yupo mahabusu kwenye gereza la Ukonga Dar es Salaam

Aliotafutwa kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Gereza Kuu Ukonga jijini Dar es Salaam, Hamis Lissu, kuhusiana na madai hayo, aliahidi kufuatilia taarifa hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na chama hicho kupitia Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema, waliodai kuzuiwa ni pamoja na John Heche, Julius Mwita, wagombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kutoka majimbo mbalimbali nchini na baadhi ya wanachama wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam.

“Walipokwenda magereza leo (jana) kwa ajili ya kumsalimia Mwenyekiti Mbowe, walizuiliwa kumwona kwa sababu ambazo magereza walisema, ‘wamepokea maelekezo kutoka juu kuwa wanaoruhusiwa ni wenye vibali tu’.

"Siku za mwisho wa wiki na sikukuu ni siku ya kutembelea wafungwa na mahabusi,” alisema.

Alisema wenye vibali wanaweza kwenda siku yoyote kama ambavyo mawakili hufanya hivyo.

“Waliomba kumwona mkuu wa gereza ila hawakufanikiwa kwa hoja kwamba yuko kwenye kikao, na hivyo wamekaa pale mpaka mchana huu walipolazimika kuondoka bila kufanikiwa kumwona na kujua ana hali gani kiafya,” Mrema alisema katika taarifa yake hiyo.

Alisema wanaendelea kuchukua hatua  mbalimbali ili wajue Mbowe ana hali gani kwa sababu siyo kawaida kwa magereza kuzuia watu kumwona mahabusi au mfungwa isipokuwa kama mtu huyo ni mgonjwa mahututi.

Chanzo: ippmedia.com