Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA waweka masharti kuelekea chaguzi hizi

Kigaila.jpeg Benson Kigaila

Sun, 26 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu mwaka 2025 kama Katiba Mpya haitapatikana.

Hayo yamesemwa  jana Jumamosi Juni 25, 2022 na naibu katibu mkuu wa Chadema, Benson Kigaila wakati akizungumza kwenye kongamano la Katiba lililofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema wameonewa vya kutosha na kwa sasa hawako tayari kuonewa tena na kwamba ukifika wakati wa chaguzi hizo kama Katiba Mpya itakuwa haijapatikana hawatashiriki chaguzi hizo.

"Tunaihitaji katiba mpya sasa, kwa sababu hatutakubali kwenda kwenye uchaguzi mkuu ujao wala uchaguzi wa serikali za mitaa bila katiba mpya, yaani kama itafika 2024 hatuna katiba mpya  na kama itafika 2025 hakuna katiba mpya, uchaguzi hautafanyika."

"Hatuna ugomvi na mtu, lakini hatuko tayari kuonewa tena, tumepuuzwa vya kutosha, tumeonewa vya kutosha kwa sasa hatuko tayari," amesema Kigaila.

Amebainisha kuwa wanahitaji katiba mpya ili kujenga taasisi imara za kusimamia utawala wa nchi na kuwa na Bunge ambalo halitakuwa sehemu ya serikali ili liweze kuisimamia serikali kikamilifu.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini,  Godbless Lema amesema wanapodai Katiba Mpya wanamaanisha itakayojibu maswali ya wananchi.

"Nimesikia CCM wanasema hatuwezi kukwepa mchakato wa katiba mpya, sasa watambue tunahitaji katiba mpya na bora kwa sababu wanaweza kukubali katiba mpya wakijua ni kitabu kipya, lakini sisi tunahitaji katiba mpya  na si yenye maandishi mapya bali  bora ambayo itaruhusu utawala bora, sheria, tume huru  na inayozingatia misingi ya haki ya binadamu".

Chanzo: www.tanzaniaweb.live