Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA walivyojipanga na mikutano ya hadhara

Chademapic Kutoshiriki CHADEMA walivyojipanga na mikutano ya hadhara

Fri, 16 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati hatima ya katazo la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa ikiwa bado haijulikani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka waliokuwa wagombea wake wa ubunge katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 kuanza maandalizi ya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yao.

Agizo hilo lilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika wakati akifungua semina ya siku mbili ya walilokuwa wagombea ubunge nchi nzima, itakayofungwa leo na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Zuio la mikutano ya hadhara liliwekwa mwaka 2016 kwa kilichoelezwa kuwa ni kutaka “wananchi wajikite kwenye shughuli za maendeleo hadi wakati wa uchaguzi”, huku likitoa ruksa kwa madiwani na wabunge pekee kwenye maeneo walikochaguliwa.

Wakati mikutano hiyo ikiwa bado kifungoni, Mnyika aliwaeleza waliokuwa wagombea ubunge wa chama hicho 2020 chini ya mwavuli wao wa ‘Bunge la Wananchi’ kuwa ni wajibu wa vyombo vya chama kuandaa mikutano ya hadhara.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa semina hiyo, Mnyika alisema: “Chadema ilifungua milango ya mazungumzo kuhusu zuio la mikutano ya hadhara ambayo ilizuiwa mwaka 2016, hata hivyo mazungumzo hayo hayajazaa matunda”.

Alisema katika kikao cha kamati kuu kilichokutana Septemba mwaka huu, miongoni mwa mambo waliyokubaliana ni pamoja na kuanza mikutano ya hadhara.

“Kafanyeni maandalizi kwenye maeneo yenu na kutoa taarifa ili chama kiweze kuanza mikutano hiyo. Ni wajibu kwa vyombo vyote vya chama kuanzia ngazi ya kanda na mabaraza kufanya maandalizi ili tujue lini tunaanza,” alisema Mnyika.

Alisema haki ya kujumuika ni haki mama kwa vyama vya siasa, hivyo ni lazima hilo isimamiwe. “Tunaendelea kudai na ni lazima haki hii ipatikane kwa njia yoyote, kwani ukitaka kuruka lazima uagane na nyonga,” alisema mtendaji mkuu wa Chadema.

Wakati Mnyika akitangaza uamuzi huo, pia kikosi kazi cha kukusanya maoni kuhusu demokrasia kwa vyama vya siasa kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na mambo mengine kilipendekeza mikutano ya vyama vya siasa iruhusiwe.

Alipotafutwa na gazeti hili jana kuzungumzia uamuzi huo, Msajili wa vyama vya siasa, Jaji Francis Mutungi alisema, asingeweza kuzungumzia hilo kwani hakuwepo katika mkutano. Hata hivyo, Jaji Mutungi alisema kuna kikao cha Baraza la vyama kinatarajiwa kufanyika, hivyo anatarajia Chadema itashiriki na itaeleza hayo.

Alipoulizwa lini kikao hicho kitafanyika, Mutungi alisema kamati ya uongozi itakutana Desemba 19 na kupanga tarehe.

“Tupo tayari” Heche ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alisema, miongoni mwa mikutano ya ndani anayoifanya maeneo mbalimbali, “ni kuwasisitiza makada wa chama hicho kujiandaa kwa mikutano.” Alisema “kwa jinsi Chadema inavyokua kama taasisi, kuwa na Chadema Digital imetusaidia sana katika njia ya mawasiliano na watu wasubiri kuona mikutano ikifanyika.”

Heche alisema, “Rais Samia kama anataka kujitofautisha na mtangulizi wake, anapaswa kusimamia Katiba na sheria za nchi inayoruhusu mikutano. Lakini mikutano ya hadhara itamsaidia yeye mwenyewe na chama chake kuona ushawishi wao kwa wananchi.”

Heche aliungwa mkono na Joseph Mbilinyi, mjumbe mwingine wa kamati kuu aliyewania ubunge Mbeya Mjini akisema, “sisi tuko tayari na kwa sasa tunaendelea na mikutano ya ndani na maandalizi yanaendelea.” Mbilinyi, maarufu kama Sugu aliyeongoza Mbeya Mjini kuanzia 2010-2020 alisema, “tumeshaanza kutesti mitambo katika maeneo mbalimbali ili tukianza mikutano tuone tuna watu, ni kweli wapo.

“Tumekwenda Tarime (Mara) watu kibao, Mulimba (Morogoro) watu wana shauku, kila tunapokwenda watu wanatusubiri na sasa tuko tayari kuanza mikutano,” alisema.

Kwa upande wake, Upendo Peneza aliyegombea ubunge Geita Mjini alisema, “tumepokea agizo la katibu mkuu na maandalizi yamekuwepo, kwani huko nyuma naibu katibu mkuu alikwisha kutangaza na tukaanza. “Tunachokisubiri ni maagizo ya mwisho ya chama, kwa sababu tunajua kuna hatua mbalimbali chama kinafanya kama majadiliano na tukishatangaziwa sisi tuko tayari,” alisema Upendo.

“Mnyika pia aliwataka makada hao kuandaa muswada wa kukwamua na kuendeleza mchakato wa Katiba. “Baada ya semina hii, undeni kamati ndogo haraka mkaandae muswada wa kudai na kuendeleza mchakato wa katiba na mijadala ya marekebisho ya sheria kuelekea uchaguzi mkuu 2025 na wa mitaa 2024,” alisema Mnyika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live