Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA, wadau siasa wakumbusha katiba mpya

KATIBA CHADEMA, wadau siasa wakumbusha katiba mpya

Tue, 20 Sep 2022 Chanzo: ippmedia.com

Pia wamesema kufungiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa nchini ni kikwazo kwa ukuaji wa demokrasia nchini.

Wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti kuhusu Wiki ya Demokrasia Duniani iliyoadhimishwa mwishoni mwa wiki, wadau hao walisema ni lazima marekebisho ya sheria yafanyike na kuwa na katiba mpya inayoendana na mazingira ya sasa.

Mchambuzi wa Siasa, Gwadumi Mwakatobe, alisema demokrasia ya nchi kwa sasa inaelekea kuzuri kwa kuwa ipo katika mchakato wa kuanza kupata katiba ya kidemokrasia ambayo ni mwongozo unaotokana na uamuzi wa wananchi.

Alisema msingi wa kidemokrasia ni kuheshimu uamuzi wa wananchi, hata kama viongozi waliopo madarakani hawatoupenda.

Alisema Tanzania haijafikia kuwa na demokrasia kamili kwa kuwa katiba iliyopo siyo ya mfumo wa vyama vingi, bali ilitokana na katiba ya chama mwaka 1977 na kuongezwa kipengele cha vyama vingi mwaka 1992.

“Mwaka 1977 hatukuwa na vyama vingi na ninakumbuka hata waliotunga katiba ya chama walikuwa watu 20 tu, akiwamo Pius Msekwa (aliyekuwa Spika wa Bunge 1994-2005). Na hawakuzunguka nchi nzima kukusanya maoni kama inavyofanyika sasa,” alisema Gwandumi.

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika, alisema Tanzania haijakomaa kidemokrasia kutokana na baadhi ya mambo yanaoendelea nchini, ikiwamo kufungia mikutano ya hadhara.

“Kwanza, serikali inatakiwa iondoe zuio la mikutano ya hadhara bila kusubiri kikosi kazi au mabadiliko ya sheria wala kanuni kwa kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa na Jeshi la Polisi vinatoa haki kwa vyama kufanya mikutano,” alisema.

Mnyika aliongeza kuwa demokrasia ya nchi inaathiriwa na kutokuwapo uchaguzi huru na haki, tume huru ya uchaguzi na uchaguzi wa kisiasa, jambo ambalo mwaka 1991 Tume ya Jaji Francis Nyalali ilipendekeza kuandikwe katiba mpya inayoelekeza kuwapo mfumo wa vyama vingi ili mambo hayo yawapo.

“Ili tujenge misingi imara ya kidemokrasia na taasisi imara, hatuna budi tuharakishe kuandika katiba mpya. Kwa kuwa siku ya kidemokrasia imepita siku chache zilizopita, serikali itoe kauli juu ya katiba, kauli ya kukamilisha mchakato wa katiba na waeleze ni lini utatungwa muswada wa sheria ya kurejesha mchakato wa katiba mpya, ili ukamilike kwa wakati kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025,” alisema Mnyika.

Mchambuzi wa siasa, Dk. Azavel Lwaitama, alisema ili nchi iwe na misingi ya kidemokrasia, uamuzi juu ya maisha ya watu unapaswa utolewe na wananchi wenyewe, jambo ambalo halijafanikiwa nchini.

“Kwa Tanzania upungufu mkubwa ni hilo la kukosekana ugatuzi wa mamlaka. Kama mtu anajiita mkuu wa mkoa, basi ukuu wake utokane na kuchaguliwa kwa utaratibu fulani. Huwezi kusema kuna demokrasia halafu mtu ambaye anashikilia maisha ya watu hajachaguliwa na watu,” alisema.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, akizungumza kwa njia ya video wakati wa kuadhimisha siku hiyo, aliyataka mataifa kudumisha demokrasia na kutilia mkazo umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari.

“Lakini kote ulimwenguni demokrasia inarudi nyuma. Raia hawashirikishwi, kutoaminiana na taarifa potofu zinaongezeka. Taasisi za kidemokrasia zinadhoofishwa.

"Sasa ni wa wakati wa kuzungumza, sasa ni wakati wa kusimama na demokrasia, maendeleo na kutetea haki za binadamu. Vyote hivyo vinategemeana na vinahitaji kuimarishwa,” alisema.

Septemba 15 mwaka huu, Tanzania iliungana na nchi zingine ulimwenguni kuadhimisha miaka 15 ya siku ya kimataifa ya demokrasia iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2007 kuhimiza serikali duniani kuimarisha demokrasia.

Chanzo: ippmedia.com