Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA na mweleko huu mpya

Samiaapic Data Mwelekeo mpya Chadema

Mon, 7 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Je, kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na mkutano wake na Rais Samia Suluhu Hassan, kutakifanya chama hicho kuzaliwa upya kupitia kampeni yake ya ‘Join the Chain’?

Hili ni miongoni mwa maswali ambayo wafuatiliaji wa siasa wanasubiri kupata majibu yake baada ya Mbowe na wenzake watatu kuachiwa huru juzi.

Mbowe alikamatwa pamoja na wafuasi wengine wa Chadema jijini Mwanza usiku wa kuamkia Julai 21, 2021 siku ambayo kulikuwa kufanyike kongamano kubwa la kudai Katiba mpya lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).

Maswali mengine ni je, nini kitafuata baada ya Mbowe kutoka? Je, atarudi kwenye mwendelezo wa madai ya Katiba?

Mbali na kampeni ya Join the Chain na mkutano wa Mbowe Ikulu, awali Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, alikutana na Rais Samia nchini Ubelgiji.

Advertisement Join the Chain

Mmoja wa viongozi wa Chadema, Godbless Lema aliwahi kunukuliwa akisema:

“Mnyororo wa “Join The Chain” umekuja kumshirikisha kila mmoja wetu katika ujenzi wa demokrasia ya kweli. Kila mtu anaweza kushiriki katika kazi hii kupitia ‘Join The Chain’, yaani Shilingi yetu Nguvu yetu. Hakuna mchango mdogo katika mapambano haya.”

Lema katika ufafanuzi wake wa ‘Join The Chain’ alisema kila mtu anao wajibu wa kushiriki mabadiliko katika nchi yake.

Alisema viongozi wa Chadema kote nchini wamekuwa mstari wa mbele usiku na mchana katika mapambano ya kutafuta usawa, haki, utawala bora na demokrasia kwa kujitolea.

Kimsingi, unaweza kusema wakati Mbowe yuko gerezani chama hicho kilikuwa hakifanyi siasa na hasa kwa wafuasi wake wengi, wakiwamo viongozi kuelekeza nguvu zao kwenye kesi hiyo.

Mbali na mwenyekiti wake kuwa gerezani, pia Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu anaishi uhamishoni baada ya kushambuliwa kwa risasi alipokuwa akihudhuria vikao vya Bunge jijini Dodoma.

Siasa za mwonekano wa nje za Chadema zilipungua nguvu na wakati mwingine kama hazikuwepo.

Kwa mujibu wa Lema, Chadema baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ilisusa kupokea ruzuku ya Serikali ikiwamo kususia matokeo ya uchaguzi wa Rais na wabunge.

Mbunge pekee wa Chadema aliyeshinda kwenye jimbo ni Aidan Kenani (Nkasi Kaskazini), wengine 19 ni wa viti maalumu, lakini wana mgogoro na chama chao.

Lema alifafanua kuwa ikiwa kila mfuasi wa chama hicho atatoa Sh1,000 kila mwezi, maana yake chama hicho kitakuwa kinapokea ruzuku kutoka kwa wa wapenzi wake takribani Sh1 bilioni kila mwezi. Bajeti yao kwa mwaka ni Sh12 bilioni.

Kwa mujibu wa Lema, Join The Chain inaongeza harakati za chama hicho kwa kuwa fedha watakazopata zitawawezesha viongozi wao kufanya shughuli za kisiasa nchini.

“Chadema ikipata bilioni moja itafanya kazi ya madai ya Katiba mpya, kujenga uelewa kwa watu, kujenga taasisi za kichama, kujenga mifumo ya kisiasa ambayo italeta ushindani katika nchi.

“Viongozi watatoka maofisini watakwenda kazini, kanda zitafanya kazi, mikoa itafanya kazi, wilaya zitafanya kazi, kata zitafanya kazi, vitongoji vitafanya kazi na vijiji vitafanya kazi,” alisema Lema alipotoa ufafanuzi wa manufaa ya Join The Chain kwenye sauti aliyoirusha mtandaoni.

Lema alisema kwa sasa viongozi wa chama hicho wanafanya kazi kwa kujitolea na kuchangishana, ikiwamo kulipia gharama za uendeshaji, mikutano na hata viongozi wa mabaraza kuna wakati hulazimika kulala kwenye magari kwa kuwa hawana fedha ya hoteli.

Join The Chain imekuja wakati kuna katazo la mikutano ya kisiasa na viongozi wa Chadema na wafuasi wao wamekumbana na rungu la dola kwa kufanya mikutano isiyo na kibali cha polisi.

Mkutano wa Rais Samia, Lissu na Mbowe

Matumaini mengine ya kuzaliwa upya Chadema mbali na Join The Chain ni mikutano miwili tofauti ya Rais SamiaSuluhu Hassan na Tundu Lissu huko Ubelgiji na mkutano wa juzi na Mbowe Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais Samia, Februari 16, 2022 akiwa mjini Brussels nchini Ubelgiji alifanya mazungumzo na Lissu na miongoni mwa mambo waliyozungumza ni kesi ya Mbowe na wenzake watatu.

Lissu akizungumza na wana habari alisema jambo la kwanza alilozungumza na Rais Samia ni kuondolewa kwa kesi ya Mbowe. Mengine ni haki za vyama vya upinzani, Katiba Mpya, maslahi ya Tundu Lissu, suala la Lissu kurejea nyumbani na wabunge viti maalumu Chadema.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu walipokutana jijini Brussels nchini Ubelgiji.

Hata hivyo, juzi baada ya Mbowe kuachiwa, alikwenda Ikulu na kuzungumza na Rais Samia.

Akizungumza baada ya kikao hicho, Rais Samia alisema waliyoongea ni umuhimu wa kushirikiana ili kuijenga Tanzania kwa kuaminiana na kuheshimiana kwa misingi ya haki.

Pia, Mbowe alimshukuru Rais Samia kwa kuonesha kwake kujali, huku akikubali kuwa msingi mkubwa wa kujenga Taifa la Tanzania ni kusimama katika haki.

Alisema wamekubaliana kufanya siasa za kistaarabu na kiungwana na kuwa yuko tayari kushirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ili nao pia waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo. Soma zaidi

Chanzo: www.tanzaniaweb.live