Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

'CHADEMA msingi' kurindima tena Dar

Chademamsingii 'CHADEMA msingi' kurindima tena Dar

Wed, 20 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema watairudia programu ya ‘Chadema msingi’ jijini hapa, shughuli itakayoambatana na kupanga safu mpya ya uongozi kuanzia ngazi ya msingi.

Mchakato huo amesema utaanza baada ya kumalizika kwa kikao cha Baraza Kuu litakaloketi Mei 11 likiwa na ajenda mbalimbali ikiwamo rufaa ya wabunge 19 waliovuliwa uanchama.

Programu ya Chadema msingi ni moja ya mbinu za kuwavutia wanachama kwa njia ya kidigitali. Pia inatumika kuwasajili wanachama wapya kuanzia ngazi ya chini. Ni wazo la Mbowe alilolipata akiwa Gereza la Segerea mwaka 2018.

Mbowe alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki iliyopita katika ziara aliyoifanya katika Jimbo la Kibamba na kukutana na wanachama na viongozi ambako alihamasisha ujenzi na uimarishaji wa chama pamoja na kusisitiza kampeni ya Join the Chain inayolenga kukusanya fedha za kukisaidia chama.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na viongozi wa mabaraza ya Chadema yakiwamo ya vijana na wanawake na viongozi waandamizi wa wilaya za Ubungo na Ilala, pamoja na wa majimbo hayo.

Katika kikao hicho, Mbowe alisema baada ya kumalizika mkutano wa Baraza Kuu la Chadema, chama kitaanza programu maalumu ya kurudia Chadema msingi kwa Mkoa wa Dar es Salaam itakayofanyika jimbo kwa jimbo, mtaa kwa mtaa.

“Safari hii tutawaandikisha wanachama wetu kieletroniki upya na kupanga safu za vuongozi kuanzia ngazi ya msingi ambayo mingi imelemaa ndani ya utawala uliopita. Tunakusudia kuifufua Chadema kwa nguvu kubwa na tutaanza na Mkoa wa Dar es Salaam.

“Kibamba mpo tayari? Tuanzie Ubungo au Mbagala? Yeyote anayetaka tuanzia kwake atuonyeshe maandalizi ili viongozi wakuu waingie mtaa kwa mtaa kuandikisha wanachama kieletroniki na kuwakabidhi kadi zao. Tunataka tumalize mitaa na kata zote za mkoa huu,” alisema.

Lengo la kuurejea mchakato huo alisema ni kuifanya Dar es Salaam kuwa ya mfano na baada ya hapo mikoa mingine itafuata. Alisisitiza kuwa hawatakwenda mikoa mingine bila kuichambua Dar es Salaam kama karanga katika programu hiyo.

“Safari hii tukifanya Chadema digital itaambatana na kujaza nafasi za uongozi, mafunzo ya wanachama kwa viongozi wetu na kukiaanda Chadema kukabiliana na changamoto zote za kisiasa,” alisema Mbowe.

Katibu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge aliwaambia wanachama wa Kibamba kuwa Chadema digital ni mpango wa muda mrefu hivyo lazima kuwekeza katika mfumo kwa kununua vifaa kama ulivyofanya uongozi wa jimbo hilo.

Kuhusu Baraza Kuu, Mbowe alisema wamesogeza mbele kikao hicho baada ya kupata mapendekezo kutoka kwa wanachama Waislamu wa chama hicho wakiwamo kutoka Zanzibar ili kukamilisha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

“Kwa sababu watakuwa wanakaribia kumaliza mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wamekiomba chama kione umuhimu wa kuutambua mwezi huu, kama ibada mahsusi kwa Waislamu. Tumeshauriana viongozi na kamati kuu ya chama na kuridhia ombi hili.

“Tumesogeza kikao cha Baraza Kuu kwa wiki mbili mbele kuruhusu wenzetu kumaliza mfungo wa Ramadhan, kusheherekea Sikukuu ya Eid El-Fitri na wale wanaofunga sita wamalize. Tukikutana Waislamu watakuwa wamemaliza mfungo na Wakristo wamemaliza Kwaresma na kazi iliyobaki ni kupambana na siasa,” alisema Mbowe.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live