Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA kuwakatia rufani makada waliofungwa

Peoples CHADEMA kuwakatia rufani makada waliofungwa

Mon, 28 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zikiwa zimepita wiki mbili tangu wananchama wanne wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Mkoani Lindi wahukumiwe kifungo chamiaka nane jela, uongozi wa chama hicho umeanza mchakato wa kukata rufaa.

Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Lindi, Idd Mandindi, aliyasema hayo katika mahojiano na Nipashe, lililotaka kufahamu hatua zinazochukuliwa katika kujaribu kuwanusuru wanachama wao waliofungwa gerezani kwa makosa ya kuharibu mali na kujeruhi watu iliyotolewa na Mahakama ya Mkoa wa Lindi.

Wanachama waliohukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mkoa wa Lindi baada ya kupatikana na hatia ya kuharibu mali wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020, ni Rajabu Hassani, Hamisi Maleje, Moshi Hamisi na Dadi Shayo, wote wakazi wa Kata ya Majengo, Halmashauri ya Mtama.

Mandindi alisema wameshaanza mchakato kwa kutoa taarifa ya kusudio hilo kwa uongozi wenzao wa kanda na hadi Taifa. Mandindi alisema licha ya kutoa taarifa ngazi ya Taifa, pia wanaendelea na taratibu za kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi Mkoa wa Lindi, kufuatilia nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi husika.

“Mchakato tayari umeanza kuwaokoa wanachama wetu waliofungwa na sasa tumefika hapa mahakamani kufuata nakala ya hukumu na mwenendo wa kesi,”alisema Mandindi.

Alipoulizwa kama wapo tayari kushirikiana na wenzao wa Chama cha ACT-Wazalendo, walionyesha nia ya kukata rufani ili kuwaokoa wanachama hao, Mandindi alisema kwamba hawapo tayari kushirikiana na chama chochote cha siasa.

Mwenyekiti huyo alisema wapo katika maandalizi ya kuwasilisha rufani yao Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, muda wowote baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika kwa mujibu wa sheria.

Februari 19, mwaka huu, wakati wa mkutano wa ACT-Wazalendo uliofanyika Mjini Lindi, mwenyekiti wake ngazi ya mkoa, Rashidi Mchinjita kwa niaba ya chama chake alitangaza nia ya kukata rufani kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Lindi dhidi ya wanachama wa CHADEMA.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live