Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA kujipambunua kwa' style' hii 2022

Chademapic Kutoshiriki CHADEMA kujipambunua kwa' style' hii 2022

Sat, 11 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chadema imepanga kuanza mwaka kwa kutekeleza majukumu sita ya kupigania uhuru, usawa na utu.

Miongoni mwa majukumu ambayo chama hicho kimejipa ni kudai “kufunguliwa kwa viongozi na wafuasi walioko magerezani katika maeneo mbalimbali pamoja na kutaka kufutwa kwa vitendo vyote vya kutisha na kuwasumbua viongozi wake.”

Akizungumza kwenye kongamano la kumbukizi ya miaka 60 ya uhuru lililoandaliwa na Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu alisema ni lazima wadai “kufunguliwa kwa vyama vya siasa vilivyofungiwa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.”

“Lazima tudai, haraka iwezekanavyo na bila masharti yoyote, kufunguliwa kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani wote walioko magerezani katika magereza mbalimbali ya nchi yetu, akiwemo kiongozi wetu na mwenyekiti wetu wa chama, Freeman Mbowe na wenzake,” alisema Lissu.

Lissu, ambaye anaishi Ubelgiji akihutubia kwa njia ya mtandao alibainisha kwamba lazima wapiganie kubadilisha mfumo wote wa utawala kwa kuwa na Katiba Mpya ili kuhakikisha viongozi hawawi na uwezo wa kuamua nani aishi na nani asiishi.

“Lazima tupiganie Katiba itakayohakikisha kwamba vyombo vya uwakilishi wa wananchi -- Bunge pamoja na Mahakama na vyombo vingine vya udhibiti wa Serikali...viwe huru kutetea haki na maslahi ya wananchi,” alisema.

Kiongozi huyo wa Chadema aliongeza kwamba lazima wapiganie mfumo mpya wa uchaguzi utakaohakikisha kuna tume huru ya uchaguzi ambayo itawezesha kupatikana kwa viongozi ambao wananchi wanawataka.

Vilevile, alisema watatengeneza mfumo ambao utawawezesha wananchi wa kawaida kupata haki ya kuishi katika nchi inayodai ubinadamu wao, mahitaji yao na masilahi yao.

“Niwape hayo ndiyo yawe majukumu ya mwaka huu wa 61 wa uhuru wetu kuanzia kesho na kwa siku zinazofuata,” alisema Lissu.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu alieleza kusikitishwa wanasherekea miaka 60 ya uhuru wakati mwenyekiti wao, Mbowe akiwa hayuko huru.

Alisema mapambano ya kudai Katiba Mpya yanaendelea na mwaka 2022 utakuwa ni wa mapambano.

“Siku kama ya leo miaka miwili iliyopita Bavicha tulichaguliwa na leo hii tunatimiza miaka miwili, ni wakati wa kutafakari kuna jambo gani jipya ambalo tumelifanya, tunapowakosoa wengine tujitathmini na sisi tulipopewa ridhaa, je, tumetenda?” alisema. Mwenyekiti wa wanachama wanafunzi (Chaso) mkoani Morogoro, Lukeregwa Rashid alisema tatizo la ajira lililopo nchini ni kwa sababu Katiba haijaweka dira ya uchumi na kwamba nchi inahitaji misingi imara, hivyo Katiba iliyopo imechoka na haiendani na mazingira.

Mratibu wa Chaso Dar es Salaam, Emmanuela Andrew alisema Katiba iliyopo inaminya demokrasia na uhuru wa kuzungumza kwa wanafunzi vyuoni.

Akizungumza na hadhira hiyo kwa njia ya mtandao, mwandishi nguli, Jenerali Ulimwengu alisema “lazima tuogope udhaifu wa aina yoyote utakaotufanya hata leo na huko tuendako kutumikishwa na watu aina yoyote watakaoweza kutubambikizia utawala wao bila wananchi kuukubali (kuporwa uhuru wetu), kwa kuwa kutawaliwa kwetu na wakoloni kulitokana na udhaifu wetu.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live