Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CHADEMA, kina Mdee ngoma nzito

Mdee Bungeniiiiiii CHADEMA, kina Mdee ngoma nzito

Sun, 15 May 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wakati Chadema ikithibitisha kupeleka barua ya kuwafuta uanachama wabunge 19 wa viti maalumu, baadhi ya wabunge hao wameibukia bungeni na wengine wakikimbilia mahakamani kupinga uamuzi huo huku uongozi wa Bunge ukisita kutoa maelezo ya uwepo wao.

Alhamisi Baraza Kuu la Chadema lilitupilia mbali rufaa za waliokuwa wanachama wake hao baada ya kukata rufaa ya kupinga uamuzi wa kufukuzwa uliofanywa na Kamati Kuu ya chama hicho mwaka 2020.

Juzi Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Benson Kigaila alipeleka barua ya chama hicho kulitaarifu Bunge kuhusu hatua hiyo.

“Barua ilipokelewa saa 2.42 asubuhi leo (jana) na Katibu muhtasi wa Spika ndiye aliyeipokea na kuisaini barua hiyo,” alisema Kigaila alipoulizwa na Mwananchi.

Hata hivyo, jana asubuhi wabunge hao walifika bungeni na kuhudhuria kikao cha Bunge huku watatu wakipewa nafasi ya kuuliza maswali na wengine kuchangia mjadala wa Bajeti ya Maji bungeni.

SOMA: Kutimuliwa kina Mdee kwaibua hoja ya Katiba

Related Kutimuliwa kina Mdee kwaibua hoja ya Katiba Hatua kwa hatua sakata la kina Mdee walivyomwagwaAdvertisement Wabunge hao waliingia mmoja baada ya mwingine tofauti na walivyoingia katika viwanja wa Bunge wote 19 wakati wa kuapishwa mwaka 2020 au walipokwenda kusikiliza hukumu ya rufaa zao wakati wa kikao cha Baraza Kuu kilichofanyika Mlimani City.

Wa kwanza kuwasili katika viwanja vya Bunge alikuwa ni Ester Matiko ambaye aliingia saa 2:50 asubuhi, akifuatiwa na Salome Makamba na kisha wengine waliingia wakati kikao kikiendelea.

Wabunge waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Matiko, Salome, Tunza Malapo, Jesca Kishoa, Annatropia Theones, Asia Mohammed na Stella Fiao.

Waliouliza maswali ni Tunza ambaye aliuliza swali kwa Waziri wa Maliasili na Utalii kujua Serikali ina mkakati gani wa kukuza utalii wa fukwe za bahari nchini.

SOMA:Hatua kwa hatua sakata la kina Mdee walivyomwagwa

Pia, wabunge wawili Salome na Asia walipewa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Bunge David Kihenzile. Baadaye Matiko alichangia hotuba ya Maji.

Akizungumza katika viwanja vya Bunge, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Haki, Kinga, Madaraka na Maadili ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka alisema kuwa amesikia suala la wabunge hao 19 kusimamishwa uanachama.

“Ninachoweza kusema ni kuwa msemaji wetu mkuu ni Spika (Dk Tulia) yeye ndiye atatuambia kuna nini kinaendelea,” alisema.

Hata hivyo, alisema wanasubiri kauli ya Dk Tulia kwa sababu yaliyotokea kule Chadema hayaji automatic (moja kwa moja) kwenye Bunge na kwamba, yeye kama mmoja wa viongozi wa kamati ya uongozi hafahamu kama taarifa imefika kwa Spika.

“Ila wenzetu (wabunge 19) tumeona wanaendelea na shughuli za Bunge na mpaka sasa tunawatambua kama wabunge hadi taarifa kuamua vinginevyo,” alisema.

Mwananchi lilipofika ofisini kwa Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi na kueleza kuwa yuko nje ya ofisi kikazi na alipopigiwa simu yake haikupokelewa.

“Please text me (tafadhali nitumie ujumbe wa maneno),” alituma ujumbe mfupi wa maneno ambapo alipotumiwa hakujibu na alipopigiwa tena simu yake iliita bila majibu.

Alipoulizwa kama amepokea barua hiyo ya Chadema, Dk Tulia alisema atazungumza baadaye.

Hata hivyo, alipoahirisha Bunge saa moja jioni aliitisha kikao cha Kamati ya Uongozi.

Mwananchi lilimfuata Matiko kuzungumza suala hilo, lakini alisema atasema muda ukifika.

Awali, taarifa zilizolifikia Mwananchi zilieleza kuwa wabunge hao wamefungua kesi mahakamani kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la Chadema. Hata hivyo, si Mahakama wala wabunge hao waliotaka kuzungumzia suala hilo kila walipotafutwa.

Itakuwaje wakishtaki?

Baadhi ya wanasheria waliozungumza na Mwananchi wameeleza majaliwa ya wabunge hao endapo watafungua mashtaka.

Naye mwanasheria maarufu nchini, Dk Onesmo Kyauke alisema suala hilo huenda likachukua muda kwani, kitakachofanyika ni kuiomba Mahakama ifanye marejeo ya kusikilizwa uamuzi wa kufukuzwa kwao.

Alisema kesi hiyo inapaswa kufunguliwa ndani ya kipindi cha miezi sita tangu walipofukuzwa, lakini kabla ya hapo wanapaswa kuwasilisha zuio kwa chama chao kuteuwa wabunge wengine kuchukua nafasi zao.

“Kama Chadema kikishateua wabunge wengine na wakaapishwa maana yake mchakato wa kesi utakuwa mrefu, unaweza kuchukua miaka kadhaa. Wanapaswa kuwasilisha zuio litakalomhusisha Spika wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),” alisema.

Alisema watapata ushindi iwapo mchakato wa kufukuzwa kwao na Baraza Kuu utaonekana kuwa na kasoro vinginevyo, mambo yatakuwa tofauti na matarajio.

Alizitaja kasoro hizo ni kutotekelezwa kwa baadhi ya haki ambazo ni kusikilizwa, muda wa kutosha wa kujitetea, maamuzi yalizingatia utetezi wao na uhalali wa wajumbe wa kikao walioshiriki kuwafukuza kwa mujibu wa Katiba ya Chadema. Tofauti na mtazamo huo, Dk Kyauke alibainisha kuwa kukosekana kwa baraza la usuluhishi wa migogoro ya vyama vya siasa nako husababisha kesi za namna hiyo kuchukua muda mrefu.

Alichokisema Dk Slaa

Akifafanua kuhusu uamuzi wa Chadema, mwanasiasa mkongwe Dk Wilbroad Slaa alisema vyama vya siasa huongozwa na katiba zao na kama uamuzi uliofanywa umefuata hilo ni sahihi.

Alieleza iwapo kuna kuridhika ama kutoridhika baada ya uamuzi huo, milango ya sheria ipo wazi hivyo wahusika wataifuata.

Alipoulizwa kama kuondoka kwa wanachama hao kuna athari kwa chama hicho Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chadema kabla ya kujiuzulu mwaka 2015, alisema kwa sababu chama kilitumia rasilimali na muda kuwajenga hadi walipofikia, kufukuzwa kwao kuna athari.

Vyama vyawakaribisha

Ingawa bado wanapambana na hawajatangaza mwelekeo mpya wa kisiasa, Mkurugenzi wa Habari wa CUF, Mohammed Ngulangwa, alisema milango ya kuwapokea ipo wazi iwapo watahitaji.

Alisema hawatasita kumpokea yeyote atakayekuwa tayari kujiunga na CUF kwa vigezo vilivyoainishwa kisheria.

“Tunapongeza sana uamuzi wa Chadema tukiamini kila chama kina taratibu zake kwa mujibu wa katiba ukiangalia hao sio wa kwanza kufukuzwa, aliwahi kufukuzwa Zitto Kabwe (wakati huo akiwa Naibu Katibu Mkuu) na leo yuko kwinginge,” alisema Ngulangwa.

Kauli hiyo inarudiwa na Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye alisema wapo tayari kuwapokea wabunge hao kama watahitaji kuungana nao.

“Hatukatai wanachama sisi ni chama cha siasa na hao ni wanasiasa, tupo tayari kuwapokea kama watakuwa tayari kujiunga na sisi,” alisema Kabwe.

Imeandikwa na Juma Issihaka, Tuzo Mapunda, Fortune Francis (Dar es Salaam), Sharon Sauwa (Dodoma).

Chanzo: www.mwananchi.co.tz