Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yazidi kutafuta usingizi Mbeya Mjini

45870 PIC+MBEYA CCM yazidi kutafuta usingizi Mbeya Mjini

Mon, 11 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Fikiria umekosa usingizi. Au umepata usingizi wa mang’amung’amu kwa siku moja. Kichwani mawazo yanakuwa kibao – mara matatizo, mikakati, mipango, furaha, mambo yaliyokushinda na mengine mengi.

Ndivyo unavyoweza kuelezea hali inayowapata viongozi na makada wa CCM katika Jimbo la Mbeya Mjini kutokana na jiji hilo kuongozwa na Chadema kuanzia ubunge, umeya na madiwani wengi.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Chadema iliigaragaza CCM kwa kunyakua Jimbo la Mbeya Mjini mara ya pili na kumfanya mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kuongoza vipindi viwili mfululizo.

Lakini, pia CCM ilijikuta inapokwa halmashauri kwenda Chadema baada ya kupoteza kata 26 kati ya 36 ambazo zilichukuliwa na Chadema katika uchaguzi huo na CCM kuambulia kata 10, kabla ya madiwani wanne waliofukuzwa Chadema kujiunga CCM na kushinda katika uchaguzi mdogo wa Novemba mwaka jana.

Kwa sasa CCM katika jimbo hilo inatumia kila njia kurudisha heshima yake kwa kunyakua mitaa mingi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika mwaka huu, kukomboa jimbo, halmashauri ya jiji na kata zote katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Pengine hali hii haiko Mbeya tu, huenda ni kwa majimbo yote yaliyochukuliwa na upinzani, lakini walau juhudi za Mbeya kuutafuta upya usingizi zinaelezwa hadharani.

Na huo ndio ujumbe mahususi wa mwenyekiti wa CCM, Mbeya Mjini, Hamphrey Msomba.

“Tunapaswa kujipanga vilivyo ili kushinda kwa kishindo katika chaguzi zijazo za Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu.”

Msomba anawaeleza wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Mbeya Mjini mikakati ya kushinda chaguzi hizo kwa kishindo, baadhi ikiwa imefanyika na nyingine ikiendelea kuandaliwa.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuhakikisha panakuwapo na uwiano sawa wanachama wa CCM na idadi ya wapiga kura. Na ili kufanikisha hilo anawataka viongozi kuanzia ngazi ya tawi hadi jimbo kuingiza wanachama wengi wapya ndani ya chama hicho.

Jambo la pili ni kuongeza uhusiano mzuri miongoni mwa viongozi wa CCM na jumuiya zake; viongozi wa CCM taasisi binafsi na za Serikali pamoja na viongozi wa CCM na wanachama.

“Tuongeze mshikamano miongoni mwa wana CCM na tusitangulize masilahi binafsi, tuache kubaguana kwa namna yoyote ile, iwe kwa dini, ukanda, ukabila kwani kufanya hivyo kutakigawa chama na kujikuta tunapoteza ushindi,” anasema katika mkakati wa tatu.

Hata kitendo cha Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kupitia taasisi yake ya Tulia Trust (TT) kutumia Sh820.39 milioni kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii katika jimbo ndani ya miaka mitatu kimewapa matumaini wana CCM, kwamba huo nao ni mkakati wa ushawishi unaokiwezesha kukubalika kwa wananchi.

Mbali na fedha hizo zilizotolewa na taasisi hiyo, Dk Tulia pia ametumia Sh93.67 milioni kwa ajili ya kuchangia ujenzi na kuimarisha CCM Mbeya Mjini na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla.

Mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais anasema fedha za mfumo huo zilisaidia katika sekta za elimu, afya, maji, miundombinu, uwezeshaji mikopo kwa vikundi na utawala huku zilile zilizotoka mfukoni mwake, Sh93.67, zikitumika kutekeleza ilani ya CCM.

Hali hiyo inamwinua Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mbalizi Road, Athman Kikeke na kutoa ya moyoni:

“CCM Mbeya Mjini ilikosa ukamilifu wa utekelezaji wa majukumu yake kwa wananchi, lakini uongozi wa sasa na kuwapata wawakilishi bungeni, Dk Tulia na Mary Mwanjelwa, naibu waziri – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, umesaidia imeanza kurudi.”

Kikeke alisema “tumeona taarifa za kila mmoja hapa wanavyofanya kazi. Hakika ni watu wa kupongezwa na kujivua Mbeya, lakini pia viongozi wetu mliopo mbele mnafanya kazi inaonekana kwa wananchi huko nje, na wanaona juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM’.

Kwa maelezo ya mjumbe huyo na ari ya mkutano huo kwa ujumla inaonekana juhudi kubwa zinafanyika ili kurejesha usingizi uliopotea kwa miaka 10.

Nje ya mkutano

Kwa sasa CCM imeanzisha utaratibu maalumu wa kufanya sensa ya kuwatambua wanachama wake kupitia mabalozi wao.

Katibu wa CCM Mbeya mjini, Gervas Ndaki anasema ofisi yake na Sekretarieti ya chama Mbeya mjini imetoa pendekezo kwa mwenyekiti wake, Hamphrey Msomba kwamba wanahitaji kufanya sensa ya wanachama walioko Mbeya mjini ambaye naye alikubaliana na wazo hilo hivyo wakaanza mchakato.

“Leo hii tunashuhudia kupata msaada wa madaftari makubwa ambayo yatawatosha mabalozi wetu wote Mbeya mjini ili kupata orodha kamili ya wanachama wetu wa CCM”.

Pia, uongozi wa chama hicho kipo kwenye harakati za kutafuta wafadhili waliotayari kukisaidia kujiweka sawa kuelekea katika chaguzi za Serikali za mitaa.



Chanzo: mwananchi.co.tz