Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yawatwisha mzigo mawaziri

B19ed8a72241a62ad519be628f7ea3d2.jpeg CCM yawatwisha mzigo mawaziri

Fri, 21 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo (pichani) amesema chama hicho kinakemea nia ovu iliyofanyika kuwakosesha wananchi umeme na kimeagiza hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.

Chongolo alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma

“Tunataka kubadilisha siasa kutoka maneno na kuwa maendeleo kwa wananchi,” alisema.

Alitoa maagizo kwa Wizara tatu ikiwemo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Nishati na Wizara ya Kilimo kuhusu kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Wizara ya Ardhi

Alisema CCM inaielekeza serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imalize migogoro ya ardhi ukiwemo umiliki wa ardhi.

“CCM kupitia ilani, inaiekekeza serikali kuhakikisha wanatatua migogoro inayohusisha mipaka ya hifadhi na wananchi, pia kutoa hati mijini na vijijini na zitumike kama dhamana kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo,” alisema Chongolo.

Alisema wanatarajia wizara hiyo itakuwa na mkakati kuonesha namna gani wamejipanga katika suala hilo na akaagiza fidia zilipwe kwa wakati ili kuepuka migogoro.

Chongolo alitaka mabaraza ya ardhi yasikilize na kutatua changamoto na yasijikite kwenye mfumo wa kutoa hukumu tu.

Wizara ya Kilimo Alisema ilani inaielekeza serikali kutoa kipaumbele kwenye kilimo cha umwagiliaji na kwamba lengo ni kuwa na hekta milioni 1.2 za kilimo hicho ifikapo mwaka 2025.

Chongolo alitaka kuwekwa kipaumbele kwenye ujenzi wa skimu za umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Pia aliitaka serikali kupitia bajeti yake ihakikishe inatoa mikopo ya pembejeo zenye masharti nafuu kwa wakulima.

Chama hicho pia kimetaka uwepo wa mfuko utakaolenga kupatikana kwa mashine za usindikaji kwenye maeneo yanayozalisha matunda kwa wingi, mbogamboga na mazao mengine.

“Kutokana na changamoto za mbegu, chama kinaagiza serikali kuongeza bajeti ya utafiti wa mbegu kama ilivyoainishwa kwenye ilani na taasisi za mbegu ziongezewe fedha ili zizalishe mbegu bora,” alisema Chongolo.

Aliitaka serikali ipange mashamba ya kimkakati ya mbegu zikiwemo alizeti na ufuta ili kuongeza kujitosheleza kwa mafuta ya kupikia.

Wizara ya Nishati

Katibu Mkuu huyo alisema, upatikanaji wa umeme wa uhakika ni jambo la lazima.

“Chama kinaonya watu wenye nia ovu juu ya suala la ununuaji wa umeme, vipato vya watu wengi viliathirika kwani wengi wanatumia umeme kuendesha shughuli zao na watakaobainika kufanya hujuma hatua kali zichukuliwe dhidi yao,” alisema.

Pia alitaka serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kukamilika kwa miradi ya umeme na kukamilika kwa wakati kwa mradi wa kuzalisha umeme wa maji katika Bwawa la Julius Nyerere.

Chongolo aliitaka serikali ihakikishe vijiji vilivyosalia vinapata umeme na hata vile vitongoji vilivyorukwa kupata umeme vinapatiwa nishati hiyo.

CCM pia iliagiza ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania mchakato wake uende kama ulivyopangwa kutokana na kuwa na manufaa makubwa kwa Taifa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz