Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yawaruka wanaonunua madaraka

F3c0b7822c32be1f12aa8129b3266db5 Abdurahman Kinana, Makamu Mwenyekiti CCM

Mon, 25 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeagiza wasimamizi wa uchaguzi ndani ya chama hicho wasimamie uadilifu na wasiwapitishe wanaonunua uongozi.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho taifa Tanzania Bara, Abdurahman Kinana alitoa maagizo hayo jana wilayani Mkuranga alipofanya ziara ya siku moja kutembelea Mkoa wa Pwani kuzungumza na viongozi wa CCM na serikali.

“Uchaguzi wa CCM unaendelea sasa tuko ngazi ya mashina, chama chetu nguvu yake iko chini sio juu ni mabalozi, matawi na kata, haya maeneo mengine ndio uongozi wa juu lakini nguvu zaidi iko chini,” alisema Kinana.

Aliwataka viongozi wa wilaya, matawi na kata kusimamia uchaguzi huo kwa haki na wasiruhushu dhuluma.

“Kuna watu wanaheshimika ndani ya chama hiki, kuna watu wanapendwa, kuna watu wanachama wanawakubali lakini fedha za kutoa hawana. Sasa viongozi nataka niwaombe uongozi haununuliwi. Umaarufu haununuliwi na kura hazinunuliwi,” alisisitiza Kinana na kuongeza:

“Anayetaka uongozi wewe omba halafu waachie wanachama waamue wenyewe. Wewe siku zote wanachama huwajui, huwatembelei, huwasalimu huna habari nao uchaguzi ukifika unaanza kupitapita unatoa hela. Kama mwenyekiti wenu wa tawi, wa kata au balozi wenu anafanya kazi nzuri muacheni aendelee na kazi hiyo,” alisema na kuongeza:

“Mimi nimechaguliwa juzi juzi kuwa Makamu Mwenyekiti, kabla ya hapo Rais (Samia Suluhu Hassan) aliniita na kuniambia anataka niwe Makamu Mwenyekiti wa CCM, nikamuambia hapo sina budi, nikavuta kalamu na karatasi tayari kupokea maagizo,” alieleza Kinana.

Alisema Rais Samia alimuagiza jambo la kwanza kuwa anataka asimamie uchaguzi wa CCM na kumtaka atoe maelekezo ili kuhakikisha unafanyika kwa uhuru na kwa haki.

“Sasa nyie mnajua nani anapitapita kutoa hela na njia nyingine ya watu kutafuta uongozi ni kuwachafua wenzao. Mtu anakaa kwenye nafasi ya uongozi au anatafuta nafasi ya uongozi halafu anazushiwa mambo ambayo hayapo,” alisema.

Kinana alisema chama hicho kinataka viongozi waadilifu na si wapenda rushwa.

“Kuchafuana hapana, kubebana hapana. Unatafuta uongozi ili upate uongozi na wewe unatengeneza matawi yako, unatengeneza watu wako viongozi wa kata ili baadaye ushinde, kwa mpango huo tutahakikisha unashindwa,” alisisitiza.

Alisema endapo mtu atapita njia isiyo halali, upo utaratibu wa chama wa kulalamika ba kuagiza kamati za siasa za mkoa na wilaya zipatiwe taarifa hizo.

“Lazima sisi tuonyeshe mfano. Tukitakataa rushwa nchini lazima tuwe mfano wa kukataa rushwa na kuwa mfano wa uadilifu ndani ya CCM,” alisema.

Aidha, aliwaomba wana CCM kutambua kuwa chama hicho ndio kilichopewa ridhaa na wananchi hivyo kina kazi nyingi, mojawapo ni kuwa na sikio la kuwasikiliza na kutatua kero zao.

Kinana alisema yeye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM ambaye ana wiki mbili tu ofisini, lakini anakutana na watu wengi na kuwasaidia kutatua matatizo.

“Hii ni moja ya kazi yangu kusikiliza watu. Mtu anahangaika huku na kule anaona bora aje kwenye chama, tuwasaidie,” alisema.

Alisema kazi nyingine ya chama hicho ni kuelezea mafanikio ya serikali na Rais.

“Pale serikali inapofanya vizuri lazima tuisemee. Serikali Kuu, wakuu wa mikoa tuwapongeze tuwape moyo nao ni binadamu sio kuwalaumu tu. Tuelezee mafanikio ya Rais wetu,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live