Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yawapasha wasiotosheka na vyeo

636e61457d22266f33306d9e23552e49 CCM yawapasha wasiotosheka na vyeo

Sun, 19 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amesema kuwa kiongozi wa ngazi yoyote serikalini asiyetosheka na wadhifa alionao, hatakaa atosheke, hata akipewa wadhifa mwingine.

Akizungumza kwenye mkutano wa utoaji wa taarifa ya utekelezwaji wa ilani ya CCM mkoani Ruvuma, ambayo alikuwa mgeni rasmi, Polepole alisema kiongozi asiyetosheka ni mwiba wa maendeleo ya chama na serikali kwa jumla.

Alisema kiongozi anayepewa madaraka na serikali kumsaidia Rais kufanya kazi fulani, lakini akaiacha na kwenda kuwania ubunge, hafai na kwamba hata akiaminiwa na kupewa tena madaraka, ataishia njiani tena.

“Yaani Rais wa nchi amekuchagua ukamsaidie kazi fulani iwe ukuu wa wilaya, mkoa au hata nafasi ya ukurugenzi mahali, kwanza ina maana amekuamini na kukuita ukasaidie kuitekeleza kazi yake hiyo. Lakini badala ya kuikamilisha wewe unaishia njiani na kisha kukimbilia kwingine, sasa wewe hutufai kabisa,” alisema.

Alisema, “Wewe badala ya kutuvusha mto, unaishia njiani na kutukimbia. Yaani watu hawa hawataacha kabisa tabia hii, ni kwa nini watu wasijifunze utii na uchapakazi kama wa Rais John Magufuli.”

Alisema kwa miaka ambayo amefanya kazi na Rais Magufuli, amebainisha kuwa anapenda kufanya kazi zaidi ya kawaida, kwa kuwa kuna wakati anashindwa kulala, kwa sababu ya kufanya kazi muda wote.

Alisema uchapakazi wa Rais Magufuli, ndiyo umesababisha afanye mambo makubwa zaidi kwa miaka mitano ya uongozi, ikilinganishwa na zaidi ya miaka 50 tangu nchi iwe huru.

Alisema Rais Magufuli amefanya hayo yote, kutokana na nidhamu kubwa aliyonayo kwa chama, kwa kuwa ndipo ulipo mwongozo wa utendaji kazi. Kauli ya Polepole kuhusu wasiotosheka na vyeo ni mwendelezo wa kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti hivi karibuni na Rais Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, ambao walikemea viongozi wasiotosheka na kuacha madaraka waliyopewa kwenda kuwania nafasi nyingine.

Katika hafla ya kuapisha viongozi Ikulu ya Chamwino, Makamu wa Rais alisema, “Mwanadamu unapoishi ni lazima utosheke na kile ulichonacho na unapokuwa hutosheki na unahaha huku na kule, Mungu ana maamuzi yake pia.”

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme alisema serikali ya Magufuli imefanya makubwa kwenye elimu, madini, afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara na uwanja wa ndege pamoja na kuimarisha sekta ya usafiri wa majini.

Kuhusu elimu, alisema serikali imewajengea vyuo viwili vya mafunzo ya ufundi stadi (VETA) katika wilaya za Namtumbo kwa gharama ya Sh bilioni nne na Nyasa kwa Sh bilioni 2.1 .

Chanzo: habarileo.co.tz