Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yawakazia wakandarasi

CCM WEB CCM yawakazia wakandarasi

Wed, 14 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, kimewataka wakandarasi wote ambao wamepewa kazi za ujenzi wa barabara mkoani humo, kuhakikisha wanakamilisha matengenezo hayo kwa wakati kulingana na mikataba.

Rai hiyo imetolewa wakati kamati ya siasa ya Chama hicho Mkoa, ilipofanya ziara kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara ya Kikweni - Vuchama ambayo inajengwa kwa kiwango cha lami kilometa 1.3 na barabara ya Kituri Proper kilometa 4.2 ambayo inajengwa kwa kiwango cha changarawe. Akizungumza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo ni vyema wale waliopewa wajibu wa kuitekeleza na kuisimamia, kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Aidha Boisafi amewataka pia wananchi kuitunza miundombinu ya barabara zinazojengwa ili kuhakikisha inakuwa endelevu kwa vizazi vya sasa na baadae. "Tumetembelea miradi mbalimbali ya Elimu, Maji, Afya na sasa tuko kwenye barabara, hakika sote tumeona kazi kubwa ambayo inafanywa na Serikali, niombe wananchi mtunze miundombinu hii, lakini pia wakandarasi mliopewa kazi mhakikishe inakamilika kwa wakati uliopangwa ili wananchi waweze kunufaika,” amesema. Ameongeza kuwa "Kila mmoja atekeleze wajibu wake na wenyeviti wa vijiji itisheni mikutano muwaeleze wananchi yale yanayofanyika na kuwasomea taarifa za mapato na matumizi kama taratibu zinavyoelekeza ili kuweka uwazi kwa wananchi." Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara ya Kikweni - Vuchama, Meneja Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema mradi huo utagharimu zaidi ya Sh1.2 bilioni na kwamba ni moja ya mikakati ya Serikali kuharakisha maendekeo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wilayani humo. Naye Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (Tarura) Wilaya ya Mwanga, David Msechu akizungumzia ujenzi wa barabara ya Kituri Proper ambayo inajengwa kwa kiwango cha Changarawe, amesema mradi huo unagharimu zaidi ya Sh490.8 milioni. "Mradi huu umeimarisha miundombinu ya barabara hivyo kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji, kuchochea shughuli za kiuchumi, kuondoa umaskini na kuwezesha huduma za kijamii kama afya na elimu," amesema Msechu. Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Kituri, wamesema kukamilika kwa barabara hiyo kutawaondolea adha mbalimbali walizokuwa wakikumbana nazo kama vile wajawazito kujifungulia njiani kutokana na kukosekan kwa miundombinu hiyo. Mbali na barabara, kamati hiyo pia ilikagua mradi wa maji wa vijiji vya Kileo na Kivulini, mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya hiyo, ujenzi wa bwalo la chakula na ukarabati wa hosteli Shule ya Sekondari Nyerere pamoja na ukarabati wa Shule ya Msingi Kifula.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live