Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yavunja ukimya Katiba mpya

A1954b594432c088ae9aa3e3611839ca CCM yavunja ukimya Katiba mpya

Tue, 15 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakina ajenda ya Katiba mpya kwa wakati huu, badala yake kipaumbele zaidi kimewekwa katika kujenga nchi kwa ukamilishaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

Pia nguvu nyingine ni katika kupambana na umaskini, kuboresha huduma za kijamii, kuboresha mazingira ya biashara, kuzidisha ustawi wa demokrasia, kusimamia utawala bora, kulinda sambamba na kuheshimu haki za binadamu.

Hivyo hakiwezi kuacha masuala hayo ya msingi yaliyobeba mustakabali wa taifa na kuanza kurudi nyuma kimaendeleo kwa maslahi ya mtu au kikundi cha watu.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo wakati akizungumza na wazee wa Wilaya ya Tanga Mjini katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga mkoani Tanga.

Shaka alisema Serikali ya ya Rais Samia inakimbizana na vipaumbele vya msingi zaidi katika maeneo mtambuka ya upatikanaji wa huduma bora za afya, utoaji wa elimu bure na bora shuleni na vyuoni, huduma za maji safi na salama zikiimarishwa katika maeneo hasa yasiyo na huduma hiyo na kuimarishwa kwa mfumo wa utoaji haki.

Nyingine ni kutoa mikopo ya riba ndogo na masharti nafuu, kuboresha kilimo na upatikanaji wa masoko ya mazao na kuweka mazingira rafiki na wezeshi kwa wafanyabishara na wawekezaji huku mkazo zaidi ukielekezwa kukomesha rushwa na ubadhirifu jambo ambalo litasaidia katika matumizi yenye tija ya utajiri wa nchi kupitia rasilimali zake.

“Hakuna mwananchi anayesema serikali iyaache yote hayo ishughulike kwanza na katiba mpya hayupo. Madai ya katiba mpya sio agenda ya kisiasa hivyo wanasiasa waache kuitumia ajenda hiyo kama turufu ya kuwahadaa wananchi kuwa hilo ndio jawabu la changamoto zao jambo ambalo sio kweli,” alisema Shaka.

Alisema taifa linahitaji viongozi waadilifu, wazalendo, wanaothamini utaifa, wanaotanguliza na kuweka mbele maslahi ya taifa ili kuwanufaisha wananchi si wanasiasa wanaoshawishi kutafuta kuungwa mkono kisiasa bila kujenga misingi madhubuti ya taasisi zao za kisiasa zinazotumika kubeba agenda hizi za wananchi.

“Watu wasipotoshe, mchakato wa kutungwa kwa Katiba mpya uliendeshwa na ulifikia hatua ya Katiba inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba ambayo inasubiri kupigiwa kura ya maoni na wananchi pale ambapo serikali itaona inafaa kukamilisha mchakato wake hivyo upinzani uache hadithi za kusadikika. Huu ni wakati wa kujenga nchi kwanza kazi ambayo CCM inaifanya baada kuaminiwa na Watanzania,” alisema Shaka.

Alisema kinachoweka chama madarakani ni sera bora, utekelezaji madhubuti, na uwezo wa kuwaunganisha wananchi katika kuwaletea maendeleo endelevu kwa usawa kama ifanyavyo CCM.

Chanzo: www.habarileo.co.tz