Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yaviita mezani vyama kujadili Katiba, maridhiano

Katibapic Data 1140x640 CCM yaviita mezani vyama kujadili Katiba, maridhiano

Thu, 16 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kipo tayari kukaa meza moja ya mazungumzo na vyama mbalimbali kwa lengo la kufanya mjadala wa Katiba pamoja na maridhiano.

Hayo yamebainishwa leo Alhamis na Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Dk Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’  katika mkutano wa Demokrasia Tanzania kwa mwaka 2024 unaofanyika katika Hotel ya Golden Tulip, ambapo amesema vyama hivyo viondoe hofu na kutoaminiana.

“Hii ni nchi yetu sote, ni lazima tuwe na maridhiano ya pamoja. Tuaminiane tufikie kwenye Katiba mpya itakayojali masilahi wetu. Sisi vyama vya siasa tukiridhiana ndiyo tukabadilishe kwa kuwa wananchi wanatusikiliza” amesema.

“Tutajenga vipi Taifa letu kama kila mmoja atakuwa na hofu?, kama hatukai pamoja hatutaweza kupiga hatua na kufikia maridhiano tunayotarajia. CCM tuko tayari kusaka Katiba mpya kwa masilahi ya Taifa letu, tunaviomba vyama vya siasa vije mezani tuzungumze na tufikie malengo tuliyokusudia,” amesema.

Dimwa amesema kuwa Katiba ni ya wote si ya vyama vya siasa hivyo ni vema wadau wote wakashirikisha kikamilifu kupitia majukwa mbalimbali.

“CCM tunaviomba vyama vya siasa virejee kwenye mazungumzo, visiende nje kueleza kile tunachojadiliana kabla ya kufikia makubaliano maana tutavuruga amani, utulivu na umoja wetu” amesema.

“CCM iko tayari baada ya uchaguzi tuendelee na mchakato wa Katiba, wapinzani waondoe hofu katika jambo hili, tukae meza moja tukubaliane ya namna ya kuijenga nchi yetu” amesema.

Dimwa amesema Katiba mpya na maridhiano yatapatikana kama vyama vya upinzani vitakuwa na dhamira njema kufanikisha mambo hayo.

Amewatupia lawama wapinzani kwa kuchangia kukwama kwa mchakato wa Katiba mpya kwa kuwa walikimbia kwenye mchakato huo mwaka 2014 katika Bunge Maalum la Katiba.

“Walipokimbia kwenye Bunge walitupa majina mabaya ambayo mpaka sasa yanatuumiza, hili la Katiba wenzetu hawakuwa na nia njema ya kuendelea nalo. Haya mabadiliko tunayoyataka muda ni mdogo wa kwenda kubadilisha Katiba, tukipita baada ya uchaguzi wa 2025 tutabadilisha Katiba na sheria ili tuipate iliyo bora zaidi”.

Dimwa amesema kuwa kama mabadiliko yote ni lazima yafanywe wote kwa pamoja kwa masilahi ya wengi.

Amesema suala la Katiba linahitaji tafakuri ya kina na kuhusisha watu wengi zaidi badala ya kudhani wanasiasa ndiyo wenye kulihodhi.

Kiongozi huyo pia amesema kuwa Katiba nzuri si suluhisho la matatizo waliyonayo wananchi bali kinachofanywa na chama chake ni kuwapelekea wananchi maendeleo ndipo yaje mengine.

Amesema kuwa maendeleo yanapopatikana kila mmoja anafurahia na ndipo inapokuja lije suala la Katiba baada ya maridhiano na kuaminiana miongoni mwao.

“Katiba si kipaumbele cha wananchi, kule Makunduchi, Konde na kwingineko wanachohitaji ni maendeleo. Hili l Katiba CCM ndiyo kinara wa mageuzi na kila mara imekuwa mstari wa mbele” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live