Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yavalia njuga viwanja vya soka

97780 Ccm+pic CCM yavalia njuga viwanja vya soka

Tue, 3 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamati Kuu ya CCM, imeunda kamati ndogo kusimamia mchakato wa kuboresha viwanja vyote vya soka vinavyomilikiwa na Chama cha Mapinduzi.

Kamati hiyo ndogo inayoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, itaanza maboresho makubwa katika viwanja 11 vilivyopo katika miji mbalimbali nchini.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alipofanya ziara katika Ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini Dar es Salaam, jana.

“Michezo ni miongoni mwa mambo ambayo tunayapa kipaumbele na ilijadiliwa katika kikao cha kamati kuu. Iko wazi idadi kubwa ya viwanja vinavyotumika ni vile ambavyo viko chini yetu

“Tayari kamati hiyo imeshakutana na watendaji wa wizara, Baraza la Michezo na rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), muda sio mrefu ukarabati mkubwa wa viwanja hivyo utaanza,” alisema Dk Bashiru.

Dk Bashiru alisema ukarabati huo utahusisha viwanja 11 vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu, Kombe la FA, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na mashindano mengine ya soka.

Pia Soma

Advertisement
“Maboresho hayo kwa kiasi kikubwa yatakuwa ya eneo la kuchezea. Tunataka angalau ile ‘pitch’ (eneo la kuchezea) iwe yenye ubora na hadhi ya juu, pia kuwe na uzio kwa usalama wa wachezaji, mashabiki na viongozi.

“Pia tunataka kuwe na uhakika wa umeme na maji. Viwe na maji ya bomba na maji ya kisima. Hilo ni jambo ambalo ni miongoni mwa yaliyojitokeza katika tume ya kuhakiki na kukagua mali za Chama,” alisema Dk Bashiru.

Katibu huyo alitaja viwanja hivyo ni Jamhuri (Morogoro), Sheikh Amri Abeid (Arusha), Mkwakwani (Tanga), Jamhuri (Dodoma), Ali Hassan Mwinyi (Tabora), Nangwanda Sijaona (Mtwara), Samora (Iringa), Liti (Singida), Nelson Mandela (Rukwa), Karume (Mara) na Kambarage (Shinyanga).

Uamuzi wa CCM kuvalia njuga ukarabati wa viwanja huenda ukawa ahueni kwa timu ambazo zimekuwa zikilalamikia ubovu wa eneo la kuchezea zikidai umekuwa ukifanya zishindwe kuonyesha kiwango bora na ushindani wa kiufundi na mbinu ndani ya uwanja.

Mara kwa mara, Bodi ya Ligi hufungia baadhi ya viwanja hasa vya Ligi Kuu Tanzania Bara na kisha kuvifungulia baada ya kufanyiwa ukarabati ingawa kumekuwa hakuna utatuzi wa muda mrefu wa changamoto hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz