Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yatoa onyo la mwisho urais Z’bar

Mon, 1 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa onyo la mwisho kwa wanachama wake wanaofanya kampeni za chini kwa chini wakiwania kumrithi Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.

Onyo hilo la mwisho limetolewa jana na kikao cha Kamati Kuu Maalumu ya Halmashauri Kuu Taifa ya CCM kilichoketi chini ya uenyekiti wa Rais John Magufuli.

Jana, taarifa ya CCM, iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole ikielezea kikao hicho cha kamati kuu maalumu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimteua Ramadhani Harlin Chande kuwa mgombea wa uwakilishi Jimbo la Jang’ombe.

Karipio la kwanza, lilitolewa Mei na Dk Shein wakati akiwa katika ziara ya kutembelea mashina ya chama hicho katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) visiwani humo akisema wana CCM walioanza kampeni mapema wanapaswa kuacha.

“Nafasi ya urais ndani ya CCM haipatikani kwa kampeni na makundi yasiyo halali, bali utaratibu maalumu kupitia vikao vya kikatiba ambavyo vipo kwa mujibu wa katiba na miongozo na kanuni mbalimbali,” alisema Dk Shein.

Rais Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema walioanza kampeni mapema wasipoacha, atawachukulia hatua kali ikiwamo kuwafikisha katika vikao vya maadili vya chama hicho ili wahojiwe na kuchunguzwa mienendo yao.

Kama hiyo haitoshi, Agosti 18, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally akiwa katika ziara ya kujitambulisha visiwani Zanzibar alizungumzia mbio hizo za urais kwa kuwaonya walioanza kampeni kabla ya wakati.

Akizungumza na wanachama wa chama hicho katika viwanja vya Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM Kisiwandui mjini Unguja, Dk Bashiru aliwatahadharisha wanachama walioanza kusaka nafasi ya urais kuwa watachukuliwa hatua za nidhamu.

Aliwaonya kuacha mbio hizo kwa kuwa muda wa kufanya hivyo haujafika, huku akiwananga baadhi yao kuwa hata udiwani hawauwezi.

Dk Bashiru alisema baadhi ya wanachama hao wameanza kuunda makundi na kupanga mikakati ya kuwania urais ikiwamo kufanya vikao vya siri na kusema kuwa utaratibu huo ni kinyume cha katiba ya chama hicho tawala.

Alisema kiongozi mzuri ni yule anayeombwa kugombea na si anayeonyesha uchu wa kusaka nafasi ya uongozi.

Alisema CCM haihitaji viongozi wa namna hiyo kwa kuwa ndiyo waliochangia kuondoa imani ya wananchi.

“Nawaomba muacheni Dk Shein amalize kipindi chake cha urais, msimbugudhi na makundi yenu,” alisema.

Suala la kuwapo kwa makundi ndani ya CCM limekuwa likijitokeza kila uchaguzi mkuu wa kubadili uongozi wa juu wa nchi unapofika.

Wakati wa mchakato wa kumpata mgombea urais wa Serikali ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 wanachama wake sita walihojiwa na kupewa onyo kwa kuanza kampeni kabla ya wakati.

Waliokumbwa na onyo hilo walikuwa Frederick Sumaye, Edward Lowassa, William Ngeleja, January Makamba, Bernard Membe na Steven Wassira. Sumaye na Lowassa baadaye walihama CCM na kujiunga na Chadema.

Hata hivyo, onyo lililotolewa na chama hicho jana halikutaja majina ya wanaCCM upande wa Zanzibar walioanza kampeni za siri ikiwamo kupanga safu zao za uongozi.

Kwa mujibu wa Katiba, Rais Shein aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza 2010 na mara ya pili 2015, huu ni muhula wake wa mwisho wa uongozi.

Kuhusu uamuzi wa kikao cha jana, Polepole alisema CCM imetoa karipio la mwisho kwa wana CCM wanaokiuka katiba, kanuni ya uchaguzi, kanuni ya uongozi na maadili,

“Kwa kuanza kufanya kampeni za kificho na za wazi za urais wa Zanzibar na kwenda kinyume na utamaduni na desturi njema za chama chetu ambazo kwa pamoja hutuongoza kuwapata viongozi wa CCM na Serikali zake.”

Akifafanua karipio hilo jana, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM- Zanzibar, Catherine Nao alisema, “Ukiona Mwenyekiti (Magufuli), Makamu Mwenyekiti (Dk Shein) na Katibu Mkuu (Dk Bashiru) wamesema unaweza kuona hali ilivyo.”

Ingawa hakutaka kuwataja majina, Nao alisema, “Yawezekana hao wanaosemwa wako serikalini au nje serikali lakini ni wana CCM. Kwa kauli hii inaonyesha wapo na wa ache kwani wanaweza kuchukuliwa hatua.”

Mbali na onyo hilo, Polepole katika taarifa yake alisema kikao hicho kilimteua Chande kuwa mgombea wa uwakilishi katika Jimbo la Jang’ombe.

Chande anakuwa mgombea katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 12 baada ya aliyekuwa mwakilishi wa jimbo hilo, Abdalla Maulid Diwani kuvuliwa uanachama wa CCM Mei 30 na kikao cha kamati kuu chini ya Rais Magufuli kutokana na kukiuka maadili ya chama.

Chanzo: mwananchi.co.tz