Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yatoa onyo kwa ‘wapigaji’

Shaka Hamdu Shaka Shaka akiwa katika harakati za ujenzji wa Chama

Mon, 16 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa kama kuna mtendaji anadhani kuwa kutakuwa na upigaji kwenye fedha za umma katika Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, basi anajidanganya.

Kimesema kuwa fedha zinazotolewa na Serikali ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni kutekeleza ahadi zilizotolewa na chama hicho katika kuwaletea Watanzania maisha bora.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Mei 16, 2022 na Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ambaye amesema wabadhirifu wa fedha na mali za umma watashughuliwa mchana.

Shaka ametoa kauli hiyo baada ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Manyara anakoendelea na ziara ya kukagua uhai wa chama hicho.

“Nataka kuwaambia kuwa wanaodhani kuna mlango wa upigaji wa fedha za umma katika Serikali ya Mama Samia basi hayo ni mawazo potofu na dhaifu sana. Serikali iko makini muda wote na inafuatilia mienendo ya mapato na matumizi ya fedha zake. Rais Samia ameteua wasaidizi ambao moja ya majukumu yao ya msingi ni kuhakikisha wanaishi na kufanyia kazi maono yake ambayo ni kuijenga nchi,” amesema Shaka.

Amesema chini ya Rais Samia, fedha nyingi za miradi ya maendeleo zimeshuka hadi ngazi za chini na matunda yake yanaonekana, hivyo ni wajibu wa kila mtu kuhakikisha fedha inayotolewa kutelekeza miradi hiyo zinatumika kama ilivyopangwa.

Advertisement Hata hivyo, Shaka ameongeza kuwa CCM hakitasita kutoa ushauri kwa serikali katika kuchukua hatua kwa mtumishi ambaye atabainika kutumia vibaya fedha za umma.

“Hapa Manyara kuna miradi mingi imetekelezwa na taarifa zilizopo fedha zimetumika vizuri na hiki ndicho tunachotaka kusikia,” amesema.

Katika hatua nyingine, Shaka amewahimiza Watanzania kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kuleta maendeleo ili kufikia Tanzania tuitakayo.

Amesema tangu ameingia madarakani Rais Samia amekuwa na uthubutu wa kufanya mambo makubwa ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na maendeleo na kwamba, hakuna shaka na uadilifu wake na kwamba ataivusha nchi salama.

Kuhusu uhuru wa kutoa maoni na mwelekeo wa kisiasa nchini, amesema kuna mabadiliko makubwa kisiasa kwa sasa tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live