Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yataka wazawa wapewe kipaumbele miradi ya ujenzi

0d98657a144636212ed1dc6dcda8fd4c CCM yataka wazawa wapewe kipaumbele miradi ya ujenzi

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora kimeiomba serikali kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa kwenye miradi ya ujenzi pindi inapotangazwa, kuwaimarisha kimitaji na uwezo na kuimarisha uchumi wa eneo husika.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Hassan Wakasuvi alitoa ombi hilo juzi alipoongoza wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa kukagua ujenzi wa barabara ya Urambo hadi Kaliua yenye urefu wa Kilometa 28, iliyojengwa na Kampuni ya Samota.

Alisema wakandarasi wazawa wanaoonesha uwezo na uaminifu katika utekelezaji wa miradi ikiwemo ya ujenzi wa barabara, wapewe kipaumbele ikiwa ni njia ya kuwaimarisha zaidi, wakue na kuweza kuomba kazi nje ya nchi.

Wakasuvi alisema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama ya mradi kwa Serikali, kwa kuwa mkandarasi wa eneo husika hakutakuwa na gharama kubwa za usafishaji wa mitambo kutoka mbali.

"Tunaomba kutoa kipaumbe kwa wazawa ili tuwe na faida nyingi ikiwemo kuwaimarisha kimitaji , ujuzi na pia hata fedha wanazopata zitabaki hapa nchini na kutoa ajira nyingi kwa wataalamu wetu wa ndani " alisisitiza.

Alitoa mwito kwa viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa na wananchi wote kuwa walinzi wa miundombinu, inayojengwa kwa kufichua wizi wa alama za barabara.

Alisema ung'oaji wa alama hizo umekuwa ukirudisha nyuma juhudi kubwa za serikali.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Samota, Salumu Abdallah aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwaamini wazawa na kuwapatia miradi ya ujenzi wa barabara kubwa ikiwamo wao ambao wanajenga barabara ya kutoka Urambo hadi Kaliua kwa gharama ya Sh bilioni 38.7.

Alisema hatua hiyo imesaidia kuwajengea uwezo na kupata ujuzi kutoka Mshauri Msimamizi ambapo hivi sasa wana uwezo wa kufanya kazi nyingine kubwa za ujenzi wa barabara kutokana mafunzo wayopata.

Abdallah alisema ni vema Serikali inapokuwa na miradi ikaweka utaratibu wa kutenga miradi ambayo wazawa wanapaswa kujenga kwa kuwa wao hawana uwezo wa kushindana kwenye zabuni na kampuni za nje ya nchi kutokana na mitaji yao kuwa kidogo ukilinganisha na wageni.

Meneja wa Mkoa wa Tabora wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Damian Ndabalinze alisema kuwa barabara hiyo ya kutoka Urambo hadi Kaliua, imekamilika kwa kiwango kikubwa na zilizobaki ni kazi ndogo ambazo zinatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.

Shughuli zilizobaki ni mifereji ya maji ya mvua, kuweka alama za kuvuka watu, kuweka mawe yanayoonyesha umbali na kuchora michoro ya usalama barabarani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz