Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yataka ujenzi wa miradi kwa staili ya fedha za Corona

Ef3f189ebba97e8601e04b83ecf97767.jpeg CCM yataka ujenzi wa miradi kwa staili ya fedha za Corona

Wed, 29 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Nyang’hwale, mkoani Geita kimeishauri serikali kuendeleza mbinu ya usimamizi inayotumika kujenga madarasa kwa fedha za Covid-19 ili miradi yote ikamilike kwa wakati.

Ushauri huo ulitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyangh’wale, Adam Mtore wakati wa kukabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule madarasa 54 ya mradi huo yaliyojengwa na Halmashauri ya Nyang’hwale.

Alisema miradi wa Covid-19 umeleta mapinduzi makubwa ya usimamizi na utekelezaji wa miradi ya umma kwani imekamilika kwa ubora na kwa wakati ikilinganishwa na miradi mingine inayochukua muda mrefu.

“Fedha nyingine zinazotolewa zisimamiwe kama hizi kumbe kila kitu kinawezekana, kwa kweli hii imetutia faraja, fedha zimetolewa Oktoba lakini leo hii tunaongelea kukabidhi majengo,” alisema.

Katibu wa CCM Wilaya ya Nyang’hwale, Chiku Masanja alisema fedha za mradi huo zimeondoa adha ya wananchi kuchangishwa kila kukicha na hivyo kutoa nafasi ya kujitolea nguvu kazi kuunga mkono.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamhuri William aliahidi kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa miradi yote ya umma na kwamba watahakikisha madarasa yote yaliyokamilika yanapata samani za wanafunzi. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Senyamule aliutaka uongozi wa halmashauri hiyo baada ya kukamilisha miradi ya madarasa sasa ihamishie nguvu kwenye mradi wa ujenzi wa vituo vya afya kwa fedha za tozo.

“Mpaka tarehe 30 Januari, wote tuwe tumekamilisha vituo vile, niendelee kutoa wito kwenu kukamilisha vituo hivyo kwa wakati, maana lengo la serikali ni wananchi kupata huduma,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live