CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza kujitoa kwa wakandarasi wa maji nchini.
Kimesema ni vyema uchunguzi huo ukaanzia Wizara ya Maji ili kujua sababu inayowafanya wakandarasi hao kuondoka na kuacha miradi mingi kabla ya kukamilika au kuanza kwa ujenzi wake.
CCM imesema kwa sasa jicho la chama hicho litakuwa katika Mradi wa Maji wa Ziwa Tanganyika kuona namna gani utekelezaji wa ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanyika kwa uhakika ili wananchi wapate huduma hiyo muhimu.
Akizungumza alipotembelea Mradi wa Maji wa Ziwa Tanganyika juzi kuona jinsi unavyotekelezwa katika kata ya Bangwe, Halmashauri ya Kigoma Ujiji, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alitaka tatizo la wakandarasi kujitoa kufanyiwa kazi.
“CCM tunaimani kubwa na nyie watendaji mliopewa dhamana ya kusimamia na jitihada hizi mnazofanya, lakini sasa mnahitaji kuongeza umakini na uzalendo, kwani mnaweza kuwa makini lakini uzalendo hamna, yapo baadhi ya maeneo hadi wakandarasi wanajitoa, kuna mambo mengi nyuma yake,” alisema. Alisema katika mradi huo wa maji wa Ziwa Tanganyika tayari mkandarasi mmoja amejitoa kufanya kazi, huku akiwa ameshafanya upembuzi yakinifu na kukubali kufanyakazi.
Awali, mradi huo ulikuwa chini ya kampuni ya Spencon Service ambayo ilijitoa katika hatua za mwanzo za ujenzi wake.
“Hapa mtu mmoja kashajitoa na huyu aliopo sasa ni wa pili, hii ni shida kubwa wakandarasi kuondoka, nilizungumza na Waziri wa Maji, Juma Aweso aliniambia anakusudia kukutana na wakandarasi nchi nzima, nadhani hili nalo muhimu.
Tunawapa kazi wakandarasi wetu tunawaamini ila sasa wanaturudisha nyuma maana kila siku tunaimba tatizo la maji ukija huku unakuta mkandarasi kajitoa,” alisema
Awali, akiwasilisha taarifa yake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Kigoma (Kuwasa), Mbike Jones alisema mradi huo unatekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Maji, ambapo imeingia mkataba na mkandarasi kampuni ya Sino Hydro Corporation kwa ajili ya ujenzi wa kitekeo kipya cha maji katika eneo la Amani Beach.
Alisema mradi huo ulitiwa saini Novemba 23, mwaka jana na kuanza kazi Julai 19, mwaka huu ukiwa chini ya wizara hiyo chini ya ufadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW).
Jonesa alisema mradi huo unatarajia kukamilika Julai 19, mwakani ambapo shughuli zinazofanyika ni ujenzi wa kituo cha kusukuma maji yasiyosafishwa chenye uwezo wa kuzalisha maji lita 42,000,000 kwa siku, ujenzi wa bwawa la muda ili kuwezesha ulazaji wa bomba la kipenyo cha milimita 1,000 la kuchukulia maji ndani ya Ziwa Tanganyika.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda alisema mradi huo umechukua muda mrefu bila kukamilika na kuwa kama utakamilika utaleta ahueni kwa wananchi na hadi sasa wameshapata Sh milioni 500 kutoka kwenye fedha za kukabiliana na ugonjwa wa Covid 19 walizopewa na Rais Samia Suluhu Hassan.