Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yataka mipango inayotekelezeka

1aa5624695d2cdf9c1b31acb2be87a55.png CCM yataka mipango inayotekelezeka

Thu, 1 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinahitaji kuona mipango ya serikali inayoleta majawabu ya changamoto kwa vitendo, badala ya mipango inayoanisha malengo mazuri lakini utekelezaji wake ni mdogo.

CCM kilisema jana kuwa, Rais Samia Suluhu ameonesha njia na utayari wa kuwa mkombozi wa changamoto za kiuchumi zikiwemo ajira kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, hivyo ni lazima aungwe mkono kwa mipango na mikakati inayotekelezeka.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo wakati akizungumza na wadau 28 kutoka taasisi za uwezeshaji nchini.

Alikutana na ujumbe huo jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo.

Kikao hicho kilichohudhuriwa na viongozi wa taasisi na mashirika ya umma na binafsi, ni sehemu ya CCM kufatilia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020 -2025.

Shaka alisema wakati umefika wa kuwa na mpango shirikishi kwa wadau hao na uwekewe uratibu mzuri wa kufanyiwa tathmini.

"Kizazi cha miaka ya 1960 kilikuwa na wajibu wa kuleta uhuru kwa nchi yetu, kizazi baada yao na sisi tukiwemo tunao wajibu wa kuleta uhuru wa kiuchumi na kuhakikisha nchi yetu inajenga uchumi wa kisasa ambao si tegemezi kupitia mapinduzi ya kilimo, ufugaji, uvuvi na viwanda kwa kutumia teknolojia, kazi kwetu kuamua kutekeleza wajibu huo au kuusaliti," alisema.

Kwa mujibu wa Shaka, sifa kubwa ya CCM ni kuwa na fikra na vitendo vya kimapinduzi, hivyo mawazo hayo yalenge kuleta maendeleo na mabadiliko makubwa na ya haraka.

“Ili kufanikisha tunahitaji sera, mipango na mikakati inayozingatia maarifa, ujuzi na teknolojia yenye kuweza kufanya mapinduzi kwenye kilimo, ufugaji, uvuvi, usindikaji na viwanda,” alisema.

Alisema Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeahidi upatikani wa ajira milioni 8 katika kipindi cha miaka 5.

Chanzo: www.habarileo.co.tz