Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yataka Chadema iombe radhi Watanzania

B1a79d11f55146393104d0a5e9c33b90 CCM yataka Chadema iombe radhi Watanzania

Thu, 6 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimekitaka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiombe radhi Watanzania kwa kuchakachua moja ya vitambulisho vikuu vya Taifa letu, Wimbo wa Taifa.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole amesema walichokifanya Chadema kimewaumiza sana CCM na wamewaachia Watanzania waamue.

“Huu wimbo tunamuomba Mungu abariki nchi hii ya Tanzania, huu wimbo hutambulisha nchi yetu ulimwenguni sambamba na jina la nchi yetu, bendera ya nchi yetu, wimbo huu ndio maana Taifa Stars wamefurahia kipindi kile wanakwenda Afcon (Kombe la Mataifa ya Afrika)…na unapoimba wimbo ule si sala ya wote”alisema Polepole wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema kuwa kila nchi inatambulishwa na vitu vitatu, likiwemo jina lake (la nchi), bendera yake na Wimbo wa Taifa, hivyo Chadema wamepunguza hadhi ya wimbo huo.

“Hiki chama mimi nimeshindwa kukielewa, nimeshindwa, yaani najaribu kutafakari nashindwa kuelewa, nidhamu ni ziro, nidhamu, hasa nidhamu ziro, kutii sheria bila shuruti ziro…halafu bila aibu wanajenga hoja tuambieni wapi tumevunja sheria”alisema Polepole na kuongeza kuwa Chadema wanashindwa kuelewa kuwa kuna sheria na lakini pia upo uhalali kwa mujibu wa makubaliano ya jamii fulani.

Alisema kuwa wimbo huo unawatambulisha Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa au kijinsia na pia unawaunganisha na Mungu wa mbinguni.

“Mimi nawaachia Watanzania, hiki ndio chama ambacho kabla hakijaomba dhamana kimeshabadili Wimbo wa Taifa na kuufanya wimbo wa chama chao…kabla hujaomba dhamana ya kuongoza nchi hii umeshabadili wimbo wa Watanzania na kuufanya wimbo wa chama chako.

Kwa hiyo Watanzania pale sijui wanabaki na nini. Hili Watanzania naliacha hili kwenu, limetuuma sana” alisema. Polepole alisema kuwa wanachofanya Chadema ni gharama ya demokrasia na angetamani Msajili wa Vyama vya Siasa azungumze lugha ya kueleweka zaidi.

“Wimbo huu si wa CCM, wimbo huu si wa Mbowe na wenzake, huu wimbo tunaimba tukiwa katikati ya vita tunaimba wimbo huu, huu wimbo tunaimba tukiwa katikati ya mapigano, huu ndio huwa kiunganishi chetu kimaombi kati ya taifa hili na Mungu wa mbinguni” alisema

Chanzo: habarileo.co.tz