Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yaonya madiwani wanaobweteka

03c3db2bdd4738bb775d7d567b8e4dc8.jpeg Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka hamdu

Mon, 30 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonya madiwani wa chama hicho waache tabia ya kubweteka. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alitoa onyo hilo wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho kwenye ofisi ya CCM Mkoa wa Lindi jana.

“Napenda kuchukua nafasi hii kuwaeleza madiwani wote wa CCM nchi nzima kujua wajibu wao, baadhi wanapokwenda kwenye mabaraza na halmashauri wanajisahu na kuweka maslahi yao mbele, nataka kuwaambia chama kinawafuatilia kujua uwajibikaji wao,” alisema Shaka.

Alisema hayo baada ya kutolewa malalamiko kutoka kwa mwanachama wa CCM kwenye mkutano huo kwamba Diwani wa eneo lao hatimizi wajibu wake. Shaka alianza ziara ya siku tatu mkoani Lindi jana kukagua uhai wa chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala.

Alisema kumekuwa na ombwe la viongozi wenye sifa ndani ya CCM na kwamba hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa. Alisema hayo baada ya mzee mwana CCM, Bakari Omar Bakari kueleza kwamba kuna tatizo la baadhi ya viongozi wa chama hicho kupungukiwa na sifa za kiuongozi na akahoji chama kinachukua hatua gani.

“Nikiri kweli kuna ombwe lakini tayari hatua zimeshachukuliwa na kuanzia hivi sasa viongozi hawa wanaochaguliwa watapatiwa mafunzo ili wawe na uwezo na elimu ya kutosha,” alisema Shaka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live