Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yampa Naibu Waziri Uvuvi siku saba kutatua kero za wavuvi

Shakapic CCM yampa Naibu Waziri siku saba kutatua kero za uvuvi

Mon, 15 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Ziara ya Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Kagera, imeanza na moto baada ya Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka kumtaka Naibu Waziri wa Uvuvi, Abdallah Ulega kwenda kutatua kero ya uvuvi.

Shaka amemtaka Ulega kwenda wilayani Bukoba ndani ya siku saba na kukutana na wavuvi na kusikiliza kero zinazowakabili wanapofanya shughuli zao kwenye Ziwa Victoria.

Pia, amewataka wana CCM kupitia uchaguzi wa Chama mwakani, wachague viongozi makini, wasio mizigo kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kukipa ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na baadaye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Shaka ameyasema hayo jana Jumapili Novemba 14, 2021 wakati akizungumza na wavuvi wa mwaro wa Rushala, Kemondo pamoja na wanachama wa mashina mbalimbali alipowatembelea katika ziara ya wajumbe wa Sekretarieti ya Chama hicho. Katika ziara hiyo ambayo itahusisha mikoa mitano lengo likiwa ni kuimarishaji uhai wa Chama kuanzia ngazi za mashina pamoja na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 -2025.

Amesema Naibu Waziri Ulega anatakiwa kukaa na wavuvi hao ili kupata ufumbuzi wa changamoto wanazokabiliwa nazo na sio kupokea ripoti zilizoandaliwa kwani, huenda zisiguse changamoto na mahitaji yao ya msingi.

Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na usumbufu kutoka kwa maofisa wa mamlaka zinazosimamia mapambano ya uvuvi haramu ambao, wamekuwa kero kubwa kwani, wanatekeleza majukumu bila kuzingatia haki.

"Nakuomba Naibu Waziri fika mkoani Kagera baada ya wiki moja ukae na wavuvi, wasikilize shida zao na zitafutiwe ufumbuzi. Ukifika hapa kutana na wavuvi wenyewe, najua utapewa taarifa zilizoandaliwa hata mimi nimepewa, lakini zipokee kisha kawasikilize wenyewe wanasemaje," Shaka amempa maagizo hayo Ulega alipozungumza naye kwa simu moja kwa moja akiwa kwenye eneo hilo na wavuvi wakisikia.

Amesema ni lazima viongozi wajue na kukubaliana naye kuwa wavuvi wana matatizo mengi licha ya kuwa eneo muhimu kwa kuzalisha ajira za vijana, hivyo Chama hakitakubali wachache wawakwamishe.

"Nimemtaka Ulega aje mwenyewe hapa na awasikilize matatizo yenu, nimekuja kutekeleza maagizo ya kuwasikiliza nimepata picha sasa ni lazima changamoto zenu zitatuliwe," amesema Shaka.

Kuhusu usalama wa wavuvi wanapokuwa ziwani, Shaka amewataka kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo husika ikiwemo Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa urahisi zaidi.

"Mtoe ushirikiano pindi mnapopata matatizo ndani ya maji ili jambo liweze kufanyiwa ufumbuzi mnapokaa kimya inakuwa sio vizuri mnapaswa kutoa taarifa,” amewaagiza.

Naye Naswiru Kamara, ambaye ni mmoja wa viongozi wa Jumuiya za wavuvi wilayani Bukoba, amesema operesheni za kupambana na uvuvi haramu zimekuwa na sura ya uonevu.

Amesema moja ya eneo ambalo utekelezaji wake ni wa kuumiza, ni ukamataji wa nyavu zisizokidhi vigezo ambao unawaumiza wavuvi wenye vyombo vikubwa.

Chanzo: mwananchidigital