Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yamjibu Mahanga, yamtaka akumbuke fadhila

14228 CCM+MAHANGA+PIC TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesikitishwa na kauli iliyotolewa na mwanachama wake wa zamani, Dk Makongoro Mahanga aliyedai alishinda ubunge vipindi viwili vya miaka 10 Jimbo la Ukonga kwa ‘kuiba kura.’

Jumamosi iliyopita katika uzinduzi wa kampeni za ubunge wa Ukonga za Chadema, Dk Mahanga aliyekuwa naibu waziri kwa miaka 10 kuanzia 2006 hadi 2015 alisema anaifahamu CCM inavyoiba kura.

“CCM nawafahamu sana, wanawatumia mabalozi kununua kadi za kupigia kura, hata mimi walikuwa wananifanyia hivyo na ninashinda. Kura zinazoibwa si za Chadema ni za wananchi, wananchi kataeni kuibiwa,” alisema Dk Mahanga, ambaye alikuwa pia mbunge wa Segerea 2010-2015.

Akijibu kauli ya Dk Mahanga, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Uhusiano wa Kimataifa, Ngemela Lubinga alisema chama hicho kimesikitishwa na kauli hiyo.

“Kwanza tunakanusha madai ya Mahanga. Pili tunasikitishwa sana na kauli hii kwa sababu yeye tulimwamini tukampa unaibu waziri kwa miaka minane. Tatu, kama CCM inaiba kura, mbona haikumwibia (Mwita) Waitara na alishinda Jimbo la Ukonga?” alihoji Lubinga.

Alipotafutwa jana kuzungumzia kauli ya Lubinga, Dk Mahanga alisema, “Unajua unaweza kuiba lakini hazitoshi, kwa hiyo kwa Waitara waliiba lakini hazikutosha kwani unaweza kuiba na zisitoshe.”

Mwananchi lilipomtafuta Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Athuman Kihamia kuhusu kauli ya Dk Mahanga alisema anayepaswa kuulizwa ni CCM. “CCM ndio wametajwa moja kwa moja na si NEC, kama tungekuwa tumetajwa NEC tungezungumza lakini sasa wametajwa CCM,” alisema.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage amewataka wasimamizi wote wa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani wa Septemba 16, wanaoshiriki mafunzo kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi.

Akifungua mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi jijini Dodoma jana aliwaonya kuacha kwenda kufanya kazi kwa mazoea ili wapunguze au kuondoa malalamiko mengi yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.

Alisema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na utaratibu unaopaswa kufuatwa na kuzingatiwa, akisisitiza hayo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi ambao hautakuwa na malalamiko au vurugu.

“Tunakutana hapa kwa siku tatu ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha kazi hii ya uchaguzi, lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi,” alisema Jaji Kaijage.

Alisema katika kipindi hiki ambacho uchaguzi mdogo unafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya kisiasa na kutoaminiana, hutawaliwa na mihemko ambayo ni chanzo cha uvunjifu wa amani.

“Ninyi mmeaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizi za usimamizi wa uchaguzi kwa kuwa mna uwezo wa kufanya kazi hii, hivyo mjiamini na kujitambua,” alisema.

Wakati huohuo, Katibu Mkuu wa Chama cha AFP, Rashid Rai amesema watamchukulia hatua kali za kisheria mgombea wao aliyeshindwa kurejesha fomu katika jimbo la Korogwe Vijijini, Abdulaziz Abdallah ikiwa watajiridhisha alirubuniwa kufanya hivyo.

Alisema utafiti wa awali walioufanya, mgombea wao kwa sababu zake binafsi alishindwa kurejesha fomu japo baadaye alisimama kuilalamikia NEC.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliovikutanisha vyama vya DP na Demokrasia Makini jana jijini Dar es Salaam, Rai alisema tangu vuguvugu la kuhama vyama lilipoanza kumeibuka genge la aliowaita wahuni wa kisiasa ambao kwa makusudi wamekuwa wakiwarubuni wagombea ili wasirudishe fomu.

Alipotafutwa Abdallah kuzungumzia suala hilo alisema zipo sababu nyingi zilizomfanya ashindwe kurejesha fomu ikiwamo malipo ya ada.

Alisema kama chama kimeamua kumchunguza na kumchukulia hatua atakapobainika kukiuka utaratibu yupo tayari.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Elias Msuya na Tumaini Msowoya

Chanzo: mwananchi.co.tz