Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CCM yakemea viongozi wasiowajibika

73e3bc61d7efcfca20a57c03bf3fa3a3.png CCM yakemea viongozi wasiowajibika

Thu, 15 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema iwapo kila kiongozi serikalini atatimiza wajibu wake na atatenda haki, changamoto zinazowakabili wananchi zitakwisha.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo alisema chama hakitakuwa na simile na viongozi na watendaji serikalini na kwenye CCM, ambao hawawajibiki.

Alisema hayo alipokuwa akihitimisha ziara ya kikazi katika wilaya za mkoa wa Mbeya na akasema tatizo lililopo ni baadhi ya viongozi 'kupiga nne' tu na kuwaacha watu wakitaabika.

Alisema hayo baada ya wananchi kulalamika kuwa wanakabiliwa na kero zikiwemo za ukosefu wa maji, dawa, masoko ya mazao, umeme, upungufu wa madarasa na madawati.

Chongolo alisema kama kila mwenye dhamana katika chama na serikalini atatimiza wajibu, matatizo mengi ya wananchi yangepata ufumbuzi.

“Watu wanahangaika kwa kukosa huduma bora, lakini tumepiga nne tu, hatuwezi kuwa na serikali ambayo haiwajibiki kutatua kero za watu,” alisema Chongolo.

Aliwaambia waliohudhuria mkutano huo wakiwemo viongozi na wataalamu wa serikali, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, kwamba katika kuelekezana na kuhimizana kuhusu utatutizi wa kero zinazowakabili wananchi, ni lazima kuwa na uelewa wa pamoja.

“Tunakwenda taratibu kwa sasa, lakini kadri siku zinavyosonga mbele, wale wanaotukwamisha lazima tuondokane nao,” alionya Mtendaji Mkuu wa CCM.

Chongolo alisema kwa viongozi na watumishi wa umma ambao wamezoea kupuuzia maagizo yanayotolewa kwa ajili ya kuwaondolea wananchi kero, waendelee na tabia hiyo.

Alisema kuna wanaodhani maagizo yanayotolewa ni porojo, lakini yeye na sekretarieti yake, wanamaanisha.“Kama mnadhani tunafanya masihara sawa, simnajua maji hayapandi mlima, kuna siku mtajua kwamba yanaweza kupanda,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz